• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Bayern Munich wakomoa PSG katika mkondo wa kwanza wa 16-bora katika UEFA ugani Parc des Princes

Bayern Munich wakomoa PSG katika mkondo wa kwanza wa 16-bora katika UEFA ugani Parc des Princes

Na MASHIRIKA

KINGSLEY Coman alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Bayern Munich dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Parc des Princes.

Bao hilo la Coman lilirejesha kumbukumbu za fainali ya UEFA 2020 ambapo tena alifunga bao la pekee na la ushindi dhidi ya PSG jijini Lisbon, Ureno, na kusaidia waajiri wake Bayern kunyanyua taji la kipute hicho.

Ingawa Kylian Mbappe aliyetokea benchi katika kipindi cha pili alifungia PSG, goli lake lilifutiliwa mbali baada ya kubainika kwamba alikuwa ameotea.

PSG ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) sasa wamepoteza mechi tatu mfululizo zilizopita katika mashindano yote.

Kwa upande wao, Bayern hawajapoteza pambano lolote tangu Septemba 17, 2022 na ushindi dhidi ya PSG unawaweka pazuri kutinga robo-fainali za UEFA msimu huu wa 2022-23. Hata hivyo, watakosa huduma za beki Benjamin Pavard katika mechi ya marudiano baada ya Mfaransa huyo kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha pili.

PSG walitumia mechi dhidi ya Bayern kumwajibisha kinda  Warren Zaire-Emery aliyeweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuanza mechi ya hatua ya muondoano kwenye UEFA akiwa na umri wa miaka 16 na siku 343 pekee.

Mfaransa huyo alizaliwa 2006, mwaka ambapo Lionel Messi, 35, alishinda taji la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia yake ya usogora akivalia jezi za Barcelona.

Baada ya vichapo viwili vya awali kutoka kwa Olympique Marseille katika kipute cha Coupe de France na AS Monaco katika Ligue 1, kuangushwa kwa PSG kunatarajiwa kumweka kocha Christophe Galtier katika presha zaidi.

PSG, ambao hawajawahi kushinda taji la UEFA katika historia, sasa wana kibarua kigumu cha kubatilisha ushindi wa Bayern watakapotua Ujerumani kwa mchuano wa mkondo wa pili mnamo Machi 8, 2023.

Huku PSG wakilenga ushindi mnono katika marudiano na kuweka hai matumaini yao ya kujizolea taji la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia, Bayern nao wana ndoto ya kutawazwa wafalme wa kipute hicho kwa mara ya saba.

Tofauti na Bayern waliokomoa VfL Bochum 3-0 katika mechi yao yao ya awali ligini, PSG walijibwaga ugani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo. Olympique Marseille waliwapepeta 2-1 katika raundi ya 16-bora ya French Cup kabla ya AS Monaco kuwacharaza 3-1 ligini.

Ingawa bado wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), vichapo vitatu mfululizo kwa sasa kunadidimiza matumaini finyu ya PSG dhidi ya Bayern waliowapiga 1-0 kwenye fainali ya UEFA mnamo 2020-21 jijini Lisbon.

Licha ya kujizolea alama sawa na Benfica (14) katika Kundi H, PSG waliambulia nafasi ya pili nyuma ya miamba hao wa Ureno kutokana na uchache wa mabao yao ya ugenini. Bayern kwa upande walishinda mechi zote sita za Kundi C lililojumuisha Barcelona, Viktoria Plzen na Inter Milan watakaoalika FC Porto mnamo Februari 22.

Pamoja na kiu ya kubamiza Bayern ugenini, PSG watapania pia kukwepa pigo la kudenguliwa kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA kwa misimu miwili mfululizo.

Kikosi hicho kilichong’olewa na Real Madrid ya Uhispania kwa jumla ya mabao 3-2 mnamo 2021-22 kwa kuchapwa 1-0 nyumbani na 3-1 ugenini, sasa kimeshinda mechi 12, kupiga sare tatu na kupoteza pambano moja kutokana na mechi 16 zilizopita nyumbani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kuitunza ngozi: Fahamu tatizo kabla ya kuchagua mbinu na...

Benfica watandika Club Bruges katika UEFA ugenini na...

T L