• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Jinsi Manchester City walivyodengua Arsenal katika kipute cha Kombe la FA

Jinsi Manchester City walivyodengua Arsenal katika kipute cha Kombe la FA

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliweka hai matumaini ya kutwaa Kombe la FA kwa mara ya saba katika historia baada ya kudengua mabingwa mara 14 Arsenal kwa kichapo cha 1-0.

Bao la pekee katika pambano hilo lililochezewa ugani Etihad lilipachikwa wavuni na beki Nathan Ake aliyeshirikiana na kiungo Jack Grealish katika dakika ya 64.

Man-City walitinga raundi ya nne ya Kombe la FA msimu huu baada ya kukomoa Chelsea 4-0 katika raundi ya tatu iliyoshuhudia Arsenal pia wakipepeta Oxford United 3-0 ugani Kassam.

Sawa na Arsenal waliotandika Manchester United 3-2 katika pambano lao la awali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Man-City nao walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-0 dhidi ya Wolverhampton Wanderers ligini.

Man-City ambao wametinga nusu-fainali za Kombe la FA katika misimu minne mfululizo iliyopita, waliepuka kuaga kipute hicho muhula huu katika raundi ya nne kwa mara ya kwanza tangu 2014-15. Sasa wameshinda mechi 10 mfululizo za Kombe la FA nyumbani na kufunga bao katika kila mchuano ugani Etihad tangu Sporting Lisbon iwalazimishie sare tasa katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 2022.

Arsenal ambao wamepita raundi ya nne ya Kombe la FA mara moja pekee tangu 2017, wanatarajiwa sasa kumakinikia zaidi vipute vya EPL na Europa League. Wafalme hao wa Kombe la FA 2019-20 walidenguliwa na Man-United katika raundi ya nne ya kivumbi hicho mnamo 2018-19 kabla ya Southampton kuwang’oa katika hatua hiyo 2020-21.

Chini ya kocha Mikel Arteta, wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL baada ya michuano 19 kwa alama 50, tano kuliko nambari mbili Man-City ambao wametandaza pambano moja zaidi. Kichapo cha Ijumaa kilikomesha rekodi yao ya kushinda mechi tano mfululizo ugenini.

Tangu wabandue Man-City kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA kwa mabao 2-0 mnamo 2019-20, Arsenal wamepoteza mechi tano mfululizo dhidi ya masogora hao wa kocha Pep Guardiola katika mashindano yote.

Hata hivyo, watakuwa na fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya Man-City katika mkondo wa kwanza wa EPL mnamo Februari 15 ugani Emirates kabla ya kurudiana Aprili 26 uwanjani Etihad.

Licha ya kuchapwa Ijumaa, Arsenal waliondolea mashabiki shaka kuhusu uwezo wao wa kuzamisha Man-City ligini kadri wanavyofukuzia taji la EPL kwa mara ya kwanza tangu 2003-04. Walidhibiti wenyeji wao katika kila idara licha ya Arteta kukifanyia kikosi kilicholaza Man-United mabadiliko sita na kupanga Martin Odegaard, Oleksandr Zinchenko, William Saliba, Gabriel Martinelli na Aaron Ramsdale kwenye benchi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bayern Munich wakabwa koo na Eintracht Frankfurt na...

Brighton wang’oa mabingwa watetezi Liverpool katika...

T L