• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Fainali ya mpira wa vikapu ya wanaume kati ya Ulinzi na KPA yaahirishwa

Fainali ya mpira wa vikapu ya wanaume kati ya Ulinzi na KPA yaahirishwa

Na AYUMBA AYODI

Mechi ya fainali ya Ligi Kuu ya mpira wa vikapu ya wanaume kati ya mabingwa watetezi Ulinzi Warriors na washindi wa zamani KPA imeahirishwa kutokana na utata.

Wanajeshi wa Ulinzi walifaa kulimana na KPA kuanzia Aprili 1 ukumbini Makande katika kaunti ya Mombasa, lakini sasa fainali imeratibiwa kung’oa nanga Aprili 16. Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) halijaeleza sababu za mabadiliko hayo ya tarehe za kuanza kwa fainali, lakini kuna uwezekano mkubwa bado halijatatua mvutano kuhusu mechi ya nusu-fainali kati KPA na Equity Bank Dumas.

Katibu wa KBF, Ambrose Kisoi alitoa ratiba ya fainali baada ya kufikia uamuzi wa kuwapa KPA ushindi dhidi ya Equity. Mechi hiyo iliyosakatwa Februari 14 ukumbini Makande ilitibuka zikisalia sekunde 59 baada ya wachezaji wa Equity kukataa kucheza kufuatia usumbufu kutoka kwa mashabiki. Wakati wa kutibuka kwa mchuano huo, KPA ilikuwa kifua mbele 66-54.

Equity ilishinda michuano miwili ya kwanza jijini Nairobi kwa alama 64-54 na 78-66 kabla ya KPA kuzoa ushindi wa mechi mbili zilizofuata ukumbini Makande 81-66 na 75-56 na kulazimisha mechi ya tano ya kuamua mshindi. Ulinzi ilitinga fainali baada ya kulemea Blades ya Chuo Kikuu cha Strathmore kwa mechi 3-0.

Katika ratiba mpya ya fainali, michuano miwili ya kwanza itachezewa Makande mnamo Aprili 16 na Aprili 17 kabla ya Ulinzi kuwa mwenyeji ukumbini Nyayo jijini Nairobi mnamo Aprili 23-25. Ulinzi ilikuwa imeomba KBF kusukuma fainali mbele kwa sababu Idara ya Majeshi itakuwa na mashindano baina ya vikosi vyake kutoka April 4-8 uwanjani Moi Air Base na pia Rais Uhuru Kenyatta atafungua rasmi kituo cha michezo cha Ulinzi katika kambi ya jeshi ya Lang’ata mnamo Aprili 14.

KPA ilishinda ligi 2014, nayo Ulinzi ikatawala 2015. Kisha, KPA ilitwaa ubingwa mwaka 2016 na kutawala ligi hadi ilipoachilia taji mwaka 2019 wakati Ulinzi ilitamba kwa michuano 3-1.

Makocha William Balozi (Ulinzi) na Samuel Kiki (KPA) walisema timu zao ziko tayari kwa fainali. Balozi alisema kuwa Ulinzi inasubiri kwa hamu kukamilisha kazi kwa kuzamisha KPA. Naye, Kiki amedai kuwa takwimu nzuri za Ulinzi dhidi yao sasa ni historia na wana hamasa ya kurejesha taji Makande.

You can share this post!

Mchujo UDA wazua hofu tele Pwani

Canada waingia fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza...

T L