• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
James Milner sasa kuchezea Liverpool hadi Juni 2023

James Milner sasa kuchezea Liverpool hadi Juni 2023

Na MASHIRIKA

NAHODHA msaidizi wa Liverpool, James Milner, ametia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja utakaomdumisha ugani Anfield kwa msimu wa nane.

Kiungo huyo raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 36, alijiunga na Liverpool bila ada yoyote mnamo 2015 baada ya kuagana na Manchester City.

Tangu wakati huo, amechezea Liverpool mara 289 na kujizolea miamba hao mataji sita, likiwemo la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la FA na League Cup.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, Milner alikubali mkataba mpya wenye mshahara uliopunguzwa pakubwa ili asalie ugani Anfield.

Sogora huyo ambaye mkataba wake na Liverpool ulikuwa ukatike rasmi mwishoni mwa Juni 2022, alikuwa na ofa za kujiunga na klabu moja ya EPL huku akiwaniwa pia na vikosi kadhaa nje ya Uingereza. Hata hivyo, alihiari kusalia Liverpool hadi mwishoni mwa msimu wa 2023.

Maamuzi ya kudumishwa kwa Milner kambini mwa Liverpool yalichangiwa pakubwa na msimamo wa kocha Jurgen Klopp aliyeshikilia kuwa asingetaka kupoteza ushawishi wa kiungo huyo aliye na uwezo wa kuwajibishwa katika idara yoyote uwanjani.

Milner alianza kusakata soka kitaaluma akiwa na umri wa miaka 16 mnamo Novemba 2002 akivalia jezi za Leeds United. Kwa kutia saini kandarasi mpya, sasa atakamilisha kipindi cha miongo miwili akinogesha soka ya EPL.

Licha ya kutowajibishwa sana katika kikosi cha kwanza, Milner alichezeshwa na Liverpool mara 24 mnamo 2021-22 na akaongoza waajiri wake kuambulia nafasi ya pili kwenye EPL, nyuma ya Man-City waliohifadhi taji la kipute hicho.

Liverpool walionyanyua Kombe la FA na Carabao Cup mnamo 2021-22, walipoteza pia taji la UEFA baada ya kuzidiwa ujanja na Real Madrid kwenye fainali iliyochezewa jijini Paris, Ufaransa mnamo Mei 28, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Wanne kati ya 58 wapitishwa kuwania urais

Raila aahidi Wakenya vitamu

T L