• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
Raila aahidi Wakenya vitamu

Raila aahidi Wakenya vitamu

NA BENSON MATHEKA

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga ameahidi kugeuza Kenya kuwa paradiso akichaguliwa rais kwenye uchaguzi mkuu Agosti 9.

Kwenye manifesto aliyozindua Jumatatu usiku, Bw Odinga anatoa ahadi tamu tamu kwa makundi yote ya Wakenya wakiwemo vijana, wazee, wanawake, walemavu, wafanyibiashara na hata Wakenya wanaoishi ng’ambo.

Bw Odinga anaahidi kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara, kufufua uchumi, kupunguza ushuru na bei za bidhaa muhimu na huduma, na kujenga viwanda katika kila kaunti akichaguliwa rais wa tano wa Kenya.

Bw Odinga pia anaahidi kufufua sekta muhimu ambazo zimeporomoka kama vile kilimo na utalii, uvuvi na ufugaji ili Wakenya wawe na maisha bora.

Kwenye manifesto aliyozindua jana, Bw Odinga anaahidi kwamba serikali ya Azimio la Umoja One Kenya itaendeleza na kukamilisha miradi iliyoanzishwa na serikali zilizotangulia huku ikiboresha maisha ya kila raia kupitia mipango ya kinga ya jamii kama Inua Jamii ambapo wakongwe na watu walio na ulemavu hutumiwa pesa kila baada ya miezi miwili.

Katika kampeni zake, waziri mkuu huyo wa zamani amekuwa akiahidi Wakenya kwamba serikali yake italipa raia maskini Sh6000 kila mwezi, ahadi ambayo amenakili katika manifesto yake.

Kando na hayo, Bw Odinga anaahidi kusaidia akina mama wasio na waume na kuhakikisha waathiriwa wa ukame watasaidiwa kikamilifu na serikali yake.

“Hakuna Mkenya anayefaa kulala njaa. Tutaongeza utoshelevu wa chakula kupitia mbinu bora za uzalishaji na uhifadhi na kwa ushirikiano wa serikali ya kitaifa na za kaunti, tutafuatilia bei za bidhaa kuzuia Wakenya kupunjwa na wafanyabiashara,” inasema manifesto hiyo.

Bw Odinga anasema iwapo Wakenya watamchagua kuwa rais wao, ataziba mianya yote inayotumiwa kupora pesa za umma zinazonyima raia huduma na maendeleo.

Aidha, anaahidi vijana nafasi za kazi na kuwapunguzia mzigo wa kufanya biashara kwa kuondoa ada na kodi wanaoanzisha ubunifu wa kutengeneza bidhaa.

“Tutachunguza viwango vya ushuru na athari zake kwa bidhaa muhimu,” asema Bw Odinga na kutaja ushuru wa ziada wa thamani kwa mafuta kama unaobebesha Wakenya mzigo mkubwa.

Kiongozi huyo wa ODM anasema kwamba serikali yake itaweka mazingira ya kuhakikisha Wakenya watapata chakula, nyumba, mavazi na mahitaji mengine ya kimsingi kwa bei nafuu.

Kando na ahadi ya kuhakikisha Wakenya huduma bora na nafuu za afya kupitia mpango wa afya wa Babacare, Bw Odinga anasema kwamba serikali yake itatoa elimu ya bure kwa watoto wote nchini.

“Elimu bora haifai kuwa ya watoto wa baadhi ya Wakenya. Chini ya serikali ya Azimio elimu itakuwa ya kila mtoto,” Bw Odinga anaahidi katika manifesto yake.

Ili kuhakikisha amepunguzia Wakenya mzigo wa gharama ya maisha, Bw Odinga anasema serikali ya Azimio itakomesha ukopaji wa madeni ghali huku akiahidi kujadili upya madeni yaliyopo. Deni ya Kenya inaelekea kutimu Sh10 trilioni na Bw Odinga anasema atahakikisha halitalipwa na vizazi vijavyo.

Bw Odinga anasema serikali ya Azimio itapitisha sheria kuunda afisi ya kusimamia madeni na itapunguza kasi ya kukopa na kufichua masharti ya kila deni iwapo italazimika kukopa.

Ahadi zingine katika manifesto ya Azimio ni kupunguza gharama ya stima ambayo imekuwa ikiumiza Wakenya na wawekezaji, kutoa hati za kumiliki ardhi kwa Wakenya wote na kugatua majukumu yote ambayo serikali ya kitaifa imekuwa ikimwamilia na kunyima pesa serikali za kaunti.

Bw Odinga anasema kwamba iwapo atachaguliwa Rais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, serikali yake itatengea serikali za kaunti asilimia 35 ya mapato ya serikali kila mwaka ili kutia nguvu ugatuzi.

Akitambua idadi kubwa ya Wakenya ni vijana, Bw Odinga ameahidi kuunda wizara itakayoshughulikia maslahi yao.

Vile vile ameahidi usalama kwa Wakenya wote ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na majangili wanaohangaisha baadhi ya maeneo nchini.

Bw Odinga anasema pia serikali yake itaimarisha mfumo wa uchukuzi na kuhakikisha haki za kila Mkenya zimeheshimiwa.

  • Tags

You can share this post!

James Milner sasa kuchezea Liverpool hadi Juni 2023

TUSIJE TUKASAHAU: Badi ahakikishe masoko yaliyogharimu...

T L