• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Kevin de Bruyne atambisha Ubelgiji dhidi ya Denmark kwenye Euro

Kevin de Bruyne atambisha Ubelgiji dhidi ya Denmark kwenye Euro

Na MASHIRIKA

NYOTA Kevin de Bruyne aliongoza Ubelgiji ya kocha Roberto Martinez kutoka nyuma na kupepeta Denmark 2-1 katika mechi ya Kundi B kwenye kampeni zinazoendelea za Euro.

Ushindi huo wa Ubelgiji wanaoshikilia nafasi ya kwanza kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), uliwawezesha kufuzu kwa hatua ya 16-bora.

Mechi hiyo iliwapa mashabiki na wachezaji wa pande zote mbili kumtumia kiungo Christian Eriksen ujumbe wa kumtakia afueni ya haraka hospitalini baada ya kupata matatizo ya moyo katika mchuano wa awali wa Kundi B uliokutanisha Denmark na Finland katika uwanja wa Parken jijini Copenhagen.

Eriksen alistahiwa mwanzoni mwa kipindi cha kwanza na mwishoni mwa kipindi cha pili huku mchezo ukisitishwa baada ya dakika 10 kuwapa maafisa wa mechi, mashabiki na wanasoka fursa ya kumpigia Eriksen makofi kwa kipindi cha dakika moja.

Mchuano ulisimamishwa katika dakika ya 10 kwa sababu Eriksen huvalia jezi nambari 10 mgongoni akichezea timu ya taifa ya Denmark.

Matukio hayo uwanjani Parken yalifanyika baada ya Yussuf Poulsen kuwaweka Denmark kifua mbele katika dakika ya pili.

De Bruyne aliletwa uwanjani mwanzoni mwa kipindi cha pili na ujio wake ukabadilisha kasi ya mchezo. Alichangia bao la kusawazisha ambalo Ubelgiji walifungiwa na Thorgan Hazard katika dakika ya 54.

Ushirikiano mkubwa kati ya Lukaku na Hazard katika safu ya mbele ya Ubelgiji ulichangia goli la pili lililojazwa kimiani na De Bruyne katika dakika ya 70.

Martin Braithwaite wa Barcelona nusura asawazishie Denmark mwishoni mwa kipindi cha pili ila kombora lake likapaa juu ya mwamba wa lango la Ubelgiji ambao kwa sasa wanajivunia alama sita kutokana na mechi mbili za Kundi B. Denmark wanavuta mkia bila alama yoyote kwa kuwa walipigwa 1-0 na Finland katika mchuano wa ufunguzi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

‘Maradona alifariki kutokana na utepetevu na mapuuza...

Kipa Buffon ajiunga upya na klabu ya Parma aliyoagana nayo...