• Nairobi
  • Last Updated May 23rd, 2024 5:49 AM
Kipkemboi, Jebet wapepea Nairobi City Marathon 2023, Tanui ahifadhi Gold Coast

Kipkemboi, Jebet wapepea Nairobi City Marathon 2023, Tanui ahifadhi Gold Coast

NA GEOFFREY ANENE

WAKENYA Robert Kipkemboi na Naomi Jebet walitikisa akaunti zao na Sh3.5 milioni baada ya kutawala makala ya pili ya Nairobi City Marathon kilomita 42, jana.

Kipkemboi alirukia uongozi zikisalia kilomita sita na kutwaa taji kwa saa 2:07:38, akifuatiwa na Charles Mneria (2:08:41) na Bernard Kipkemoi (2:09:24).

Jebet aliibuka malkia kwa saa 2:24:33 baada ya kuchupa kileleni kilomita ya 37. Alifuatiwa na Sharon Chelimo (2:25:20) na Judith Jeruth (2:27.01).

Washikilizi wa nafasi 20 za kwanza katika mtimko huo walipokea zawadi za fedha ikiwemo Sh3.5 milioni, Sh2.2m na Sh1.5m kwa waliobuka tatu-bora, mtawalia.

Katika makala ya mwaka jana, washindi Brimin Misoi na Agnes Barsosio walivuna Sh6.9m kila mmoja.

Kitengo cha 21km wanaume, Mganda Maxwell Rotich aliwika kwa saa 1:00:10 akifuatiwa na Wakenya Vincent Kipkorir (1:01:18) na Kennedy Kimutai (1:01:24).

Nafasi tatu-bora kinadada ziliendea Gladys Chepkurui (1:09.06), Susan Chembai (1:10.05) na Nancy Chepleting (1:10:17).

Nafasi tatu za kwanza 10km zilinyakuliwa na Peter Mwaniki (dakika 28:10), Hillary Chepkwony (28:15) na Shadrack Kipchirchir (28:26).

Kinadada bora walikuwa Brenda Tuwei (31:59), Miriam Chepkech (32:15) na Miriam Chebet (32:34) mtawalia.

Kwenye mbio hizo zilizovutia washiriki 15,000 — zilizoanzia barabara ya Douglas Wakiihuri na kumalizikia ndani ya uwanja wa kitaifa wa Nyayo baada ya kuzuru barabara mbalimbali jijini Nairobi — kulikuwa pia na kitengo cha kilomita sita cha limbukeni walioshiriki tu kujifurahisha.

Mawaziri Kipchumba Murkomen (Uchukuzi) na Ababu Namwamba (Michezo), Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Katibu Peter Tum (Michezo) walihudhuria makala hayo ya Nairobi City Marathon.

Kwingineko, katika mbio za Gold Coast Marathon nchini Australia, Wakenya Rodah Tanui (2:27:10) na Ruth Chebitok (2:28:17) walizoa nafasi mbili za kwanza wakifuatiwa na mwenyeji Genevieve Gregson (2:28:33).

Chebitok na Tanui ni washindi wa Gold Coast mwaka 2018 na 2019, mtawalia.

Mkenya wa kwanza katika kitengo cha wanaume alikuwa bingwa wa Singapore Marathon 2022, Ezekiel Omullo, aliyeimarisha muda wake bora kutoka 2:08:41 hadi 2:08:26 akimaliza katika nafasi ya pili.

Nambari moja hadi tatu walituzwa Sh2.1 milioni, Sh1.0m na Sh562,400, mtawalia.

Aidha, Shirikisho la Riadha Kenya (AK) limealika wanariadha 160 kwa mchujo utakaofanyika Ijumaa na Jumamosi wiki hii uwanjani Nyayo.

Mchujo huo utakuwa wa kusaka wawakilishi wa Kenya kwenye Riadha za Dunia zitakazoandaliwa Agosti 19-27 jijini Budapest, Hungary.

  • Tags

You can share this post!

Kijana wa miaka 15 afariki baada ya kugusa waya wa umeme

Miaka minne baadaye: John Demathew aliuawa?

T L