• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Miaka minne baadaye: John Demathew aliuawa?

Miaka minne baadaye: John Demathew aliuawa?

NA MWANGI MUIRURI

MASWALI kuhusu kifo cha aliyekuwa nabii wa usanii katika jamii za Mlima Kenya, Bw John Demathew yanaendelea kuulizwa tunapoelekea kuadhimisha miaka minne tangu azikwe.

Kuna mashabiki wake ambao hawajawahi kuamini kwamba ajali iliyomuua karibu na mji wa Thika mnamo Agosti 18, 2019 haikuwa imepangwa.

Mkuu wa kitengo cha Trafiki eneo la Thika Magharibi wakati huo Bi Elenah Wamuyu alitangaza kwamba gari la Bw Demathew liligonga lori lililokuwa kwa mwendo karibu na Mkahawa wa Blue Post, unaomilikiwa na familia ya Jomo Kenyatta.

Bw James Karega ambaye amezindua harakati za kusaka ukweli kwa niaba ya mashabiki wa Demathew sasa anasema kuna mengi yalifichwa kuhusu ajali hiyo.

Aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “kifo hicho kilifanyika katika Kaunti ya Murang’a, lakini polisi walioamrishwa kutoa taarifa kuihusu ni wa Kaunti ya Kiambu”.

Aliongeza kwamba “mashahidi waliojitokeza katika eneo la ajali dakika chache tu walionekana kwa tabia na matamshi kama waliokuwa na habari kwamba Demathew angeangamia mahali hapo”.

Maswali tata kuhusu kituo cha polisi gari la Demathew lilipelekwa

Aidha, Bw Karega alisema kwamba baada ya ajali, gari la mwendazake lilivutwa hadi kituo cha polisi cha Makuyu kilichoko eneobunge la Maragua–Kilomita tano kutoka eneo la mkasa.

“Ajali ilitokea katika eneobunge la Gatanga na ambapo kuna vituo vya polisi kama Ndururumo na Kirwara. Thika bado kuna kituo cha polisi na ndipo palikuwa karibu. Lakini gari hilo lilivutwa na likapita eneobunge la Kandara ambapo kuna stesheni ya Kabati, halikuwekwa katika kituo cha Ngati,” akasema.

Karega alisema kwamba mauti ya Bw Demathew yalishughulikiwa kwa haraka isiyoeleweka kiasi cha kusemwa yalisababishwa na uendeshaji gari kiholela ili kumnyima uchunguzi sauti mbadala ya kusema huenda aliuawa.

“Hata iwe ni miaka mingapi tutangoja…Ni lazima siku moja ukweli utajitokeza. Mungu aliyembariki Demathew na talanta yake na akamjaalia kupendwa na wengi atajileta tu na aweke mauti hayo wazi kila mtu ashuhudie ukweli,’ akasema.

Bw Demathew alikuwa amehudhuria hafla ya kuchangisha pesa kusaidia mtoto wa msanii mwenzake, Bw Kigia wa Esther aliyekuwa akiugua.

Alisemwa kwamba alitumia mvinyo na ghafla saa za giza akaamka, akaingia kwenye gari lake na akatoka kwa hafla hiyo kabla ya kukumbana na mauti yake kilomita moja baadaye.

“Ripoti ya upasuaji wa mwili ilisema kwamba kuna chembechembe za damu, mkojo na mate pamoja na zingine kutoka kwa tumbo, mafua na maini ambazo zilitwaliwa ili kutekeleza uchunguzi zaidi wa kimaabara,” alisema.

Aliongeza kuwa hadi waleo, matokeo hayajawahi kutolewa kwa umma ili kuelezea hali aliyokuwa “wengi tukishuku akijipata kwa ajali hiyo huenda alikuwa amepoteza fahamu aidha kutokana na sumu au dawa za kumlaza”.

Akifahamika rasmi kama Bw John Ng’ang’a Mwangi, alikuwa amejipa ufuasi wa dhati katika jamii za Mlima Kenya ambapo alikuwa akitoa utabiri na mwelekeo katika ngoma zake.

Bw Demathew aliaga dunia wakati siasa kati ya Tangatanga na Kieleweke zilikuwa zimechacha, Kieleweke ukiwa mrengo wa Uhuru Kenyatta na Tangatanga ukiwa wake William Ruto.

Bw Demathew alikuwa ametoa msimano wake kuwa wa kumuunga mkono Bw Ruto, akiachilia ngoma: Twambe Turihe Thiri (kwanza tulipe deni).

Katika wimbo huo, alimsifu Bw Ruto kama aliyesaidia Uhuru Kenyatta kutwaa urais katika chaguzi za 2013 na 2017 na hivyo kuweka jamii za Mt Kenya katika deni la kumsaidia Ruto kurithi urais katika uchaguzi wa 2022.

Isitoshe, Kenyatta alikuwa ametoa kauli ya “yangu kumi na ya Ruto 10” na ambayo Demathew alisema ni deni.

Akiaga, kulikuwa na ishara tosha kwamba rais Kenyatta na wandani wake walikuwa wamebadilisha mawazo kuhusu ufaafu wa Bw Ruto kurithi urais na badala yake walikuwa wakimpendelea Bw Raila Odinga.

Bw Demathew alikuwa amezindua kampeni za kuuza urithi wa Ruto Ikulu katika Kaunti ya Embu na alikuwa amepanga ratiba ya kuzidisha kampeni hizo katika Kaunti za Nairobi, Murang’a, Kiambu, Nyandarua, Nakuru, Laikipia, Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga na Nyeri.

Lakini akaaga dunia huku mrengo huo wake wa kisiasa ukipambana kufa kupona na ukaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kipkemboi, Jebet wapepea Nairobi City Marathon 2023, Tanui...

Samidoh analenga kiti cha kisiasa 2027?

T L