• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Kocha Mwalala apigwa kalamu Homeboyz FC

Kocha Mwalala apigwa kalamu Homeboyz FC

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Kakamega Homeboyz Cleophas Shimanyula amesema kuwa sasa analenga kumsajili kocha wa haiba kutoka nchini au raia wa kigeni ili kujaza pengo la Bernard Mwalala.

Shimanyula jana Jumatatu alimfuta kazi Mwalala na kutema baadhi ya maafisa wa benchi ya kiufundi wa Kakamega Homeboyz kutokana na kile alichosema ni ukosefu wa nidhamu na kupuuza majukumu yao.

Afisa huyo alisema kuwa ni mkufunzi wa makipa pekee David Juma ndiye hakutimuliwa, na sasa ndiye atasimamia mazoezi ya timu hiyo.

“Mwalala, naibu wake na wanachama wengine wa benchi ya kiufundi wameachishwa kazi kutokana na ukosefu wa nidhamu na kupuuza majukumu yao,” akasema Shimanyula.

“Unaweza kuwa kocha mzuri lakini ukikosa nidhamu hutaenda popote,” akaongeza.

Shimanyula alisema kuwa Homeboyz sasa imekuwa kati ya timu kubwa KPL na atahakikisha anapata mkufunzi wa haiba kutoka hapa nchini au ng’ambo kuchukua usukani.

“Tunalenga kocha mzuri kutoka raia wa kigeni au hata hapa nchini na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi. Kwa sasa David Juma atainoa timu hadi tumpate kocha mpya,” akasema Shimanyula.

Mwalala, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Harambee Stars, aliongoza Homeboyz kumaliza katika nafasi pili nyuma ya mabingwa Tusker.

Homeboyz na Tusker wote walimaliza ligi na alama 63, ila vijana wa kocha Robert Matano walikuwa na ubora wa mabao manne.

Hata hivyo, Abana ba Ingoo walitunukiwa alama za bure katika mechi mbili za mwisho baada ya FC Talanta na Kariobangi Sharks kukosa kufika uwanjani.

Huu ulikuwa msimu wa pili Mwalala akisimamia Homeboyz kwa kuwa alikuwa naibu wa kocha Nicholas Muyoti msimu wa 2020/21.

Muyoti alipojiunga na Nairobi City Stars mwanzoni mwa msimu jana, Shimanyula alimpandisha Mwalala ngazi hadi kuu kocha mkuu.

Awali alihudumu kama kocha wa Bandari kati ya 2018-2020 na Nzoia mnamo 2016-2017. Aliongoza Bandari kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia mara mbili. Pia alifikisha timu hiyo katika hatua ya mwondoano ya Kombe la Mashirikisho mnamo 2019.

Katika taifa jirani la Tanzania, Mwalala anahusudiwa sana na mashabiki wa Yanga baada ya kung’aa akiwachezea enzi zake.

  • Tags

You can share this post!

DKT FLO: Je, uzito kifuani huletwa na nini?

Kibra Girls yawaka moto ligi ya KWPL ikielekea ukingoni

T L