• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Lukaku afunga bao lake la 67 katika mechi ya 100 ndani ya jezi ya Ubelgiji

Lukaku afunga bao lake la 67 katika mechi ya 100 ndani ya jezi ya Ubelgiji

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku, 28, alisherehekea mechi yake ya 100 ndani ya jezi ya timu ya taifa ya Ubelgiji kwa kufunga bao lake la 67 lililowezesha timu hiyo kukomoa Jamhuri ya Czech 3-0 katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Lukaku ambaye ni fowadi matata wa Chelsea, alitikisa nyavu za wageni wao katika dakika ya nane baada ya kupokezwa krosi safi na Hans Vanaken.

Vanaken alichangia pia bao la pili la Ubelgiji ambalo lilifumwa wavuni na kiungo mvamizi wa Real Madrid, Eden Hazard mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Bao la Hazard lilikuwa lake la kwanza kimataifa tangu Novemba 2019.

Ushirikiano mkubwa kati yake na Lukaku lilichangia bao la tatu lililofungwa na kiungo Alexis Saelemaekers katika dakika ya 65.

Lukaku ndiye mwanasoka wa sita kuwahi kufikisha mechi 100 akiwajibikia timu ya taifa ya Ubelgiji. Hata hivyo, angali na mechi nyingi mno kufikia rekodi ya mapambano 132 ambayo yametandazwa na sogora nambari tano, Jan Vertonghen ambaye bado ni tegemeo katika safu ya ulinzi ya kikosi hicho kinachoshikilia nafasi ya kwanza duniani kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA).

Kwa kuwa alionyeshwa kadi nyingine ya manjano dhidi ya Czech, Lukaku atakosa mechi ya Jumatano itakayokutanisha Ubelgiji na Belarus nchini Urusi.

Ushindi dhidi ya Czech uliwadumisha Ubelgiji kileleni mwa Kundi E kwa alama 13 kutokana na mechi tano. Ni pengo la pointi sita ndilo linatamalaki kati yao na Czech wanaoshikilia nafasi ya pili. Wales ambao wanajivunia alama sita, bado wana mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na vikosi hivyo viwili vya kwanza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Polisi wakabiliane na sarakasi za siasa

Salah ataka Liverpool wamfanye sogora ghali zaidi wa EPL...