• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Lukaku: Ilibidi tuzoee maziwa na mkate kila siku kwa sababu ya msoto nyumbani

Lukaku: Ilibidi tuzoee maziwa na mkate kila siku kwa sababu ya msoto nyumbani

CECIL ODONGO Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI wa Ubelgiji Romelu Lukaku amesimulia namna kwao walilelewa kwa maisha ya umaskini mkubwa na jinsi usakataji wake wa kabumbu ulivyomsaidia kubadilisha hali hiyo.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30 kupitia chapisho lililotundikwa kwenye na Twitter na @Football—Tweet mnamo Jumatano alisema maisha hayo ya dhiki yalimpa msukumo wa kujituma katika soka.

“Nilikuwa na umri wa miaka sita na nikija kupata chamcha, chakula kilikuwa kile kile; mkate na pakiti ya maziwa. Hatukuwa na pesa na mamangu alikuwa akichanganya maziwa na maji kisha tunakula na mkate,” akasema Lukaku, ambaye amekuwa akisakatia Inter Milan kwa mkopo kutoka Chelsea.

Katika sehemu kubwa ya simulizi hilo ilikuwa dhahiri kuwa mwanadimba huyo aliishi kwa umaskini mkubwa japo kwa sasa ni kati ya wachezaji wanaoogelea kwenye bahari ya pesa.

Alizungumzia jinsi ambavyo hata kumudu gharama ya umeme kulikuwa kibarua kizito, alivyokuwa akiogeshwa na mamake kwa maji ya kupasha moto na jinsi walivyokopa mikate kutoka kwa duka moja la kuoka mikate kisha kulipa baadaye.

“Waokaji mikate walinijua mimi na ndugu yangu. Kwa hivyo, walikuwa wakiniruhusu kuchukua mikate Jumatatu kisha tungelipa Ijumaa. Nilifahamu kuwa tulikuwa tumelemewa na umaskini na mamangu hangeweza kukimu mahitaji yetu,” akaongeza Lukaku.

“Kuna siku nilitoka shule na kumpata mama akilia. Hatimaye nilimwaambia mambo yatabadilika. Nilimsisitiza kuwa nitacheza soka kwa klabu ya Anderlecht na tutakuwa sawa. Hutakuwa na wasiwasi tena,” akasema.

Ndoto ya kuchezea Anderlecht ilitimia kwa kuwa alichezea ‘Under 17’, kabla ya kuhamia Chelsea mnamo 2011

Lukaku kwa sasa ana utajiri ambao unakadiriwa kuwa Sh21.7 bilioni. Hata hivyo, bado kuna vuta nikuvute na Chelsea na Inter Milan kuhusu iwapo timu hiyo ya Italia itamsajili kwa kandarasi ya kudumu.

  • Tags

You can share this post!

Magaidi wa Al-Shabaab wazidiwa nguvu na walinzi wa Kenya...

Karen Nyamu: Kupata dhahabu ni rahisi kuliko mwanamume

T L