• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Man-City wakomoa Newcastle na kukalia vizuri kileleni mwa jedwali la EPL

Man-City wakomoa Newcastle na kukalia vizuri kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walikomoa Newcastle United 4-0 ugani Etihad na kufungua mwanya wa alama tatu kati yao na nambari mbili Liverpool waliokabwa koo na Tottenham Hotspur kwa sare ya 2-2 ugenini.

Ushindi wa Man-City dhidi ya Newcastle ulikuwa wao wa nane mfululizo ligini na mabao yao yalifumwa wavuni kupitia Ruben Dias, Joao Cancelo, Raheem Sterling na Riyad Mahrez ambaye sasa ana magoli 50 katika EPL akivalia jezi za Man-City.

Kufikia sasa, Man-City ndicho kikosi cha pekee cha EPL ambacho kimefungwa idadi ndogo zaidi ya mabao (tisa) huku wakitikisa nyavu za wapinzani mara 44 kutokana na mechi 18. Ingawa hivyo, tofauti ya mabao yao (35) inawiana na ile ya Liverpool ambao wamecheka na nyavu za wapinzani mara 50 baada ya kuokota mipira kimiani mara 15.

Licha ya kubebesha Newcastle gunia la mabao, Guardiola hakuridhishwa na mchezo wa kikosi chake. “Tulicheza vibaya katika kipindi cha kwanza. Tulipoteza mpira kirahisi na vijana hawakuonana vyema uwanjani. Newcastle wangalitufunga mabao mengi ya mapema lakini nao wakasuasua,” akatanguliza Guardiola.

Man-City sasa watasherehekea Krismasi wakiselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa mara nyingine. Mara zote walipofaulu kufanya hivyo mnamo 2011-12 na 2017-18, waliishia kutawazwa wafalme wa taji la kipute hicho.

Man-City sasa wanashikilia rekodi ya kushinda idadi kubwa zaidi ya mechi za EPL (34) mwaka huu wa 2021. “Rekodi zinaashiria uthabiti wa kikosi. Lengo letu si kushinda tu mataji kwenye fainali. Tunacheza tukiwa na msukumo wa kushinda kila mchuano ndiposa tunavunja na kuweka rekodi,” akasema Guardiola.

Man-City walipoteza mechi mara ya mwisho mnamo Oktoba 30 baada ya Crystal Palace kuwapepeta 2-0 ugani Etihad. Tangu wakati huo, wamelaza Manchester United, Everton, West Ham, Aston Villa, Watford, Wolves, Leeds na Newcastle huku wakifunga mabao 24 na kuruhusu wapinzani kutikisa nyavu zao mara tatu pekee.

Mnamo 2020-21, Man-City walishinda mechi 15 mfululizo ligini na kujizolea taji la tano la EPL katika kipindi cha misimu 10. Newcastle ya kocha Eddie Howe ilishuka dimbani ikiwa na rekodi duni ya kupoteza mechi 10 za awali dhidi ya Man-City. Sasa wanakamata nafasi ya 19 kwa pointi 10 sawa na Norwich City wanaovuta mkia.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Newcastle 0-4 Man-City

Wolves 0-0 Chelsea

Tottenham 2-2 Liverpool

You can share this post!

Wolves wakaba Chelsea koo katika EPL ugani Molineux

Spurs na Liverpool nguvu sawa katika EPL

T L