• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
Wolves wakaba Chelsea koo katika EPL ugani Molineux

Wolves wakaba Chelsea koo katika EPL ugani Molineux

Na MASHIRIKA

KASI ya Chelsea kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ilipigwa breki na Wolves waliowalazimishia sare tasa uwanjani Molineux mnamo Jumapili.

Ombi la Chelsea kutaka mechi hiyo iahirishwe kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi mapya ya corona lilitupiliwa mbali Jumapili asubuhi. Maamuzi hayo yaliweka Chelsea katika ulazima wa kupanga wanasoka wanne pekee kwenye benchi japo kikosi cha kwanza kilikuwa thabiti na imara.

Hata hivyo, mabingwa hao wa 2016-17 walizidiwa maarifa na Wolves katika takriban kila idara na wakasajili sare kwa mara ya pili mfululizo ligini. Bao la Daniel Podence wa Wolves mwanzoni mwa kipindi cha pili lilifutiliwa mbali kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Leander Dendoncker naye alimtatiza pakubwa kipa wa Chelsea, Edouard Mendy huku mlinda-lango wa Wolves, Jose Sa naye akifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Christian Pulisic katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Chelsea sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 38, sita nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Manchester City walioponda Newcastle United 4-0 ugani St James’ Park. Wolves kwa upande wao walisalia katika nafasi ya nane kwa alama 25, moja nyuma ya Tottenham Hotspur walioambulia sare ya 2-2 dhidi ya Liverpool.

Wolves ndicho kikosi kilicho na idadi ndogo zaidi ya mabao katika mechi za EPL nyumbani kufikia sasa msimu huu. Chelsea kwa upande wao sasa wameshinda mechi moja pekee kutokana na nne zilizopita ligini.

Jorginho, Ruben Loftus-Cheek, Kai Havertz na Andreas Christensen walikosa kuunga kikosi kilichotegemewa na Chelsea dhidi ya Wolves. Mechi sita kati ya 10 za EPL zilizokuwa zisakatwe wikendi ziliahirishwa kutokana na janga la corona.

Manchester United vs Brighton, Southampton vs Brentford, Watford vs Crystal Palace, West Ham vs Norwich, Aston Villa vs Burnley na Everton vs Leicester ni mechi za EPL zilizoahirishwa wikendi.

You can share this post!

Real Madrid na Cadiz waumiza nyasi bure katika La Liga...

Man-City wakomoa Newcastle na kukalia vizuri kileleni mwa...

T L