• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Man-City waponda Leeds United na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

Man-City waponda Leeds United na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliruka Liverpool na kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupepeta Leeds United 4-0 mnamo Jumamosi usiku ugani Elland Road.

Man-City walishuka dimbani wakiwa na ulazima wa kutandika Leeds ili kuwapiku Liverpool waliodhibiti kilele kwa muda mfupi baada ya kukomoa Newcastle United 1-0 mapema Jumamosi.

Huku ushindi wa Man-City ukiweka hai matumaini yao ya kuhifadhi taji la EPL, matokeo hayo yaliweka Leeds ya kocha Jesse Marsch katika hatari ya kuteremshwa ngazi ligini mwishoni mwa msimu huu.

Man-City walifungua karamu ya mabao kupitia kwa Rodri aliyeshirikiana na Phil Foden katika dakika ya 13 kabla ya Nathan Ake kupachika wavuni goli la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Foden alichangia pia bao la tatu ambalo Man-City walifungiwa na Gabriel Jesus katika dakika ya 78 kabla ya beki Ruben Dias kuchangia bao la nne lililojazwa kimiani na Fernandinho sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Man-City kwa sasa wanajivunia alama 83, moja nyuma ya nambari mbili Liverpool wanaofukuzia rekodi ya kutwaa mataji manne katika kampeni za msimu mmoja. Mbali na EPL, Liverpool ambao tayari wamenyanyua ubingwa wa Carabao Cup, bado wanafukuzia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA.

Kocha Pep Guardiola aliwasaza benchi wanasoka Kevin de Bruyne, Bernardo Silva na Riyad Mahrez kadri anavyokiandaa kikosi chake kwa mkondo wa pili wa nusu-fainali ya UEFA dhidi ya Real Madrid ugenini mnamo Mei 4, 2022. Man-City watajibwaga ugani wakijivunia ushindi wa 4-3 katika mkondo wa kwanza ugani Etihad.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Newcastle 0-1 Liverpool

Aston Villa 2-0 Norwich

Southampton 1-2 Crystal Palace

Watford 1-2 Burnley

Wolves 0-3 Brighton

Leeds 0-4 Man-City

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Chelugui awarai wafanyakazi wadumishe amani msimu wa...

Mshahara wa chini kabisa sekta ya umma waongezwa kwa...

T L