• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Ronaldo aweka rekodi ya ufungaji mabao na kusaidia Man-United kupepeta Arsenal ligini

Ronaldo aweka rekodi ya ufungaji mabao na kusaidia Man-United kupepeta Arsenal ligini

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao lake la 800 kitaaluma kabla ya kufuma wavuni penalti iliyowavunia waajiri wake Manchester United ushindi wa 3-2 dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Alhamisi usiku ugani Old Trafford.

Man-United walitoka nyuma na kushinda kipute hicho kilichotawaliwa na maamuzi mengi yenye utata licha ya kurejelewa kwa teknolojia ya VAR.

Mchuano huo ulihudhuriwa pia na kocha mshikilizi wa Man-United, Ralf Rangnick pamoja na nahodha wa zamani wa kikosi hicho, David Beckham.

Emile Smith Rowe aliwaweka Arsenal kifua mbele katika dakika ya 13 kabla ya juhudi zake kufutwa na Bruno Fernandes mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Arsenal walifungiwa bao la pili na Martin Odegaard kabla ya Ronaldo kuzamisha chombo cha wageni wao kwa magoli mawili ya haraka kunako dakika za 52 na 70 mtawalia.

Mbali na Ronaldo, wanasoka wengine wanaojivunia rekodi ya kuwahi kufunga zaidi ya mabao 800 kitaaluma ni nyota wa zamani wa Janhuri ya Czech, Josef Bican (821) na nguli wa Brazil, Pele (zaidi ya mabao 1,000).

Rangnick anatarajiwa kushikilia mikoba ya Man-United hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22 na anafuata wakufunzi David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer katika juhudi za kurejesha uthabiti waliokuwa wakijivunia mabingwa hao mara 20 wa EPL chini ya kocha Sir Alex Ferguson aliyestaafu 2013.

Man-United wanavaana na Crystal Palace katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Disemba 5 huku Arsenal wakiendea Everton ugani Goodison Park siku moja baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ramaphosa afokea mataifa ya Afrika yanayotenga Afrika Kusini

Mzee aenda kortini kudai pesa kutoka kwa mwanawe

T L