• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 10:55 AM
Manchester City wapiga Chelsea na kujiweka pazuri kuhifadhi ubingwa wa EPL

Manchester City wapiga Chelsea na kujiweka pazuri kuhifadhi ubingwa wa EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walijiweka pazuri kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kutandika Chelsea 1-0 ugani Etihad, Jumamosi.

Kiungo Kevin De Bruyne ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea ndiye alifungia Man-City bao la pekee na la ushindi katika pambano hilo.

Nyota huyo raia wa Ubelgiji alimwacha hoi kipa Kepa Arrizabalaga aliyeaminiwa fursa ya kujaza nafasi ya Edouard Mendy aliyeitwa na Senegal kambini mwao kuunga kikosi cha fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon.

Ushindi dhidi ya Chelsea ulikuwa wa 12 mfululizo kwa Man-City kusajili na sasa wanajivunia rekodi ya kuchapa wapinzani mara 18, kuambulia sare mara mbili na kupoteza michuano miwili kati ya 22 iliyopita ligini.

Man-City wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 56 huku pengo la pointi 13 likitamalaki kati yao na nambari mbili Chelsea. Nambari tatu Liverpool watawaruka Chelsea na kutua nafasi ya pili mnamo Januari 16, 2022 iwapo watazamisha chombo cha Brentford watakaomenyana nao ugani Anfield.

Liverpool kwa sasa wanakamata nambari ya tatu jedwalini kwa alama 42. Nafuu kwa wapambe hao waliotawazwa wafalme wa EPL 2019-20 chini ya mkufunzi Jurgen Klopp ni kwamba wana mechi mbili zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo tayari imesakatwa na Man-City na Chelsea.

Man-City watavaana na Southampton ugenini katika mchuano ujao ligini kabla ya kualika Fulham kwa pambano la raundi ya nne ya Kombe la FA. Baada ya hapo, watakuwa na mswaki dhidi ya Brentford na Norwich City kabla ya ubabe wao kutiwa kigezoni.

Kikosi hicho kinachofukuzia mataji matatu muhula huu, kitamenyana na Sporting Lisbon ya Ureno katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Februari 15 kabla ya kupepetana na Tottenham Hotspur, Everton na Manchester United kwa usanjari huo ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kutengeneza supu tamu ya malenge...

Sababu ya Aubameyang kukosa mechi ya Gabon dhidi ya Ghana

T L