• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Namwamba: Tutakata mabilioni ya Safari Rally hadi nusu

Namwamba: Tutakata mabilioni ya Safari Rally hadi nusu

Na AYUMBA AYODI

SERIKALI inapanga kupunguza bajeti ya raundi ya Mbio za Magari za Dunia (WRC) Safari Rally hadi nusu.

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba amesema kuwa Sh2.6 bilioni zilizotolewa na serikali kwa makala yaliyopita “zimepita kiasi kabisa”, na kuongeza kuwa Kamati ya uendeshaji na Kamati andalizi zinaweza kuandaa mashindano ya kufana kwa kutumia bajeti ndogo.

Makala ya 70 ya Safari Rally yataandaliwa Juni 22-25 katika kaunti za Nairobi na Nakuru.

“Tunaamini tunaweza kuandaa Safari Rally ya kufana tukiwa na bajeti ndogo,” alisema Namwamba na kuongeza kuwa wanaunda miongozo itakayoangaliwa na kamati zote mbili.

“Tumewapa miongozo na tunataka waiangalie na kutoa mapendekezo ama ushauri wa kukata bajeti,” alisema Namwamba, akisisitiza wanaweza kufanya mengi na bajeti ndogo.

Alifichua kuwa amempa Mhasibu Mkuu wa Serikali Nancy Gathungu miezi mitatu kuangalia akaunti za makala ya Safari Rally 2022.

“Hatutaki kumpa masharti kwa sababu ni kazi ya kawaida anayofanya. Hata hivyo, tumemuomba asipitishe siku 60,” alisema Namwamba hapo Jumatatu wakati wa kuzindua kamati za uendeshaji na andalizi za Safari Rally katika jumba la Maktaba Kuu, Nairobi.

Waliohudhuria ni pamoja na mwenyekiti wa kamati andalizi Carl “Flash” Tundo na katibu wa kamati ya uendeshaji Phineas Kimathi ambaye pia ni mwenyekiti wa Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF).

Namwamba alisema kila kitu kiko shwari baada ya mazungumzo ya kufana na KMSF, Shirikisho la Mbio za Magari za Kimataifa (FIA) na mapromota wa WRC juma lililopita.

“Tunataka kusafisha mchezo huu na kuuendesha kwa njia ya wazi,” Namwamba aliambia wanakamati na kuongeza kuwa, Kenya haitaona matunda mazuri kupitia mazungumzo na uhusiano usio mzuri.

Namwamba alidokeza kuwa mabadiliko aliyofanya katika kamati andalizi yanalenga kuleta mawazo na mtazamo mpya kuhakikisha Safari Rally inakuwa bora na kutaka kamati hizo zifanye kazi kwa pamoja.

Alisema kuwa maafisa walioteuliwa walistahili na anaamini makala ya 2023 yatakuwa bora kuliko mawili yaliyopita.

Namwamba alisifu aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na KMSF kwa kupigania kurejeshwa kwa Safari Rally katika ratiba ya WRC baada ya miaka 19.

Aliongeza kuwa Rais William Ruto ameapa kuhakikisha kuwa Safari Rally itasalia katika kalenda ya WRC.

Wakati huo huo, Namwamba amesema anaangalia bajeti ya Sh6 milioni ya raundi ya Mbio za Magari za Afrika (ARC) Equator Rally iliyowasilishwa kwake. Sikh Union imechukua majukumu ya kuandaa Equator Rally mnamo Machi 17-19 mjini Voi katika kaunti ya Taita-Taveta.

“Mwanzoni, tulikuwa tumepewa bajeti ya Sh200 milioni kwa shindano hilo na inaonesha kuwa tukiwa na mipangilio bora, tunaweza kutumia fedha kidogo na kufanya kazi kubwa,” alisema Namwamba.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE 

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa PSG baada ya Neymar kupata jeraha dhidi ya Lille...

Barcelona wakomoa Cadiz na kufungua mwanya wa alama nane...

T L