• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Pigo kwa PSG baada ya Neymar kupata jeraha dhidi ya Lille katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa

Pigo kwa PSG baada ya Neymar kupata jeraha dhidi ya Lille katika mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa

Na MASHIRIKA

SOGORA Neymar Jr aliondolewa uwanjani kwa machela kabla ya Lionel Messi kufunga bao la ushindi katika dakika ya 95 kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ulioshuhudia waajiri wao Paris Saint-Germain (PSG) wakipepeta Lille 4-3, Jumapili.

PSG walikuwa wakiongoza kwa 2-0 kabla ya Lille kufunga mabao ya haraka kupitia kwa Bafode Diakite, Jonathan David na Jonathan Bamba na kufanya mambo kuwa 3-2.

Kylian Mbappe, aliyefungulia PSG ukurasa wa mabao, alipachika wavuni goli lake la pili katika dakika ya 87 na kuwarejesha waajiri wake mchezoni.

Bao hilo lilibadilisha kasi ya mchezo na Messi akajaza kimiani bao la ushindi baada ya kuvurumisha kombora kutoka hatua ya mita 20.

Licha ya ushindi huo muhimu, pigo kubwa kwa PSG ni jeraha la kifundo cha mguu linalotarajiwa kumweka Neymar nje ya kikosi chao kwa muda mrefu.

Nyota huyo wa zamani wa Barcelona alionekana akiwa katika maumivu makali akiondolewa uwanjani Parc des Princes huku akifunika uso wake kwa mikono.

Hata hivyo, ni matarajio ya kocha Christophe Galtier kwamba Neymar atakuwa amepona kabisa kufikia Machi 8, 2023 wakati wa mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Bayern Munich.

PSG watatua Ujerumani kwa ajili ya gozi hilo wakiwa na kibarua kizito cha kubatilisha ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Bayern dhidi yao katika mkondo wa kwanza nchini Ufaransa.

Ushindi wa PSG ulikomesha msururu wa matokeo duni yaliyowashuhudia wakipoteza mechi tatu mfululizo. Sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 57, tano zaid kuliko nambari mbili Olympique Marseille waliotandika Toulouse 3-2.

PSG walishuka dimbani dhidi ya Lille wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kupigwa na Marseille 2-1 katika hatua ya 16-bora ya French Cup kisha kutandikwa 3-1 na AS Monaco katika Ligue 1 na kupepetwa 1-0 na Bayern kwenye UEFA. PSG walidhalilisha Lille kwa kichapo cha 7-1 katika pambano la mkondo wa kwanza wa Ligue 1 msimu huu nyumbani mnamo Agosti 2022.

Kabla ya Neymar kupata jeraha, PSG tayari walikuwa bila mwanasoka Nuno Mendes ambaye pia alipata jeraha baya la mguu. PSG watashuka ugani kwa mara nyingine mnamo Februari 26 kuvaana na Marseille katika Ligue 1 ugenini.

MATOKEO YA LIGUE 1 (Jumapili):

PSG 4-3 Lille

Brest 1-2 Monaco

Lorient 3-0 Ajaccio

Rennes 2-0 Clermont

Troyes 0-1 Montpellier

Lens 3-1 Nantes

Toulouse 2-3 Marseille

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Real Madrid wakomoa Osasuna na kuendelea kuifuata Barcelona...

Namwamba: Tutakata mabilioni ya Safari Rally hadi nusu

T L