• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Olunga aongoza Al Duhail kutwaa ubingwa wa Qatar Cup

Olunga aongoza Al Duhail kutwaa ubingwa wa Qatar Cup

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIZI Michael Olunga alinyakua taji lake la pili msimu huu wa 2022-2023 baada ya kuongoza Al Duhail kupiga Al Sadd 2-0 kwenye fainali ya Qatar Cup ugani Jassim Bin Hamad mnamo Alhamisi usiku.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya alifungua ukurasa wa magoli dhidi ya mahasimu hao wa tangu jadi katika dakika ya 48 alipokamilisha krosi safi kutoka kwa Ferjani Sassi.

Kiungo Sassi kutoka Tunisia aliongeza bao la pili dakika ya 53 katika mechi hiyo ambayo Olunga alipumzishwa dakika ya 89 na nafasi yake kutwaliwa na Ismail Mohamad.

Olunga alinyakua taji lake la kwanza msimu huu wakati Al Duhail almaarufu Red Knights walinyuka Umm Salal 1-0 katika fainali ya Qatar Stars Cup mnamo Machi 28.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 yumo mbioni pia kushinda Ligi Kuu. Timu yake iliyo chini ya kocha Hernan Crespo kutoka Argentina, inaongoza ligi hiyo ya klabu 12 kwa pointi 42 baada ya kujibwaga uwanjani mara 17.

Olunga anaongoza katika ufungaji wa mabao kwenye ligi hiyo baada ya kucheka na nyavu mara 14.

Mechi ijayo ya Al Duhail ni robo-fainali ya Emir Cup dhidi ya Al Sailiya mnamo Aprili 10.

  • Tags

You can share this post!

Ramadhani yazidi kunoga mji na mitaa hailali usiku

Azimio yateua wakali meza ya majadiliano

T L