• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ronaldo aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao katika Kombe la Dunia na kusaidia Ureno kupepeta Ghana katika Kundi H

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ronaldo aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao katika Kombe la Dunia na kusaidia Ureno kupepeta Ghana katika Kundi H

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga bao katika fainali tano za Kombe la Dunia baada ya kusaidia Ureno kukomoa Ghana 3-2 katika mechi ya Kundi H ugani 974 Stadium, Qatar.

Ronaldo ambaye sasa amevunja rekodi za Pele, Uwe Seeler na Miroslav Klose kwa kufunga bao katika makala matano tofauti ya Kombe la Dunia, alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu ashiriki mahojiano yaliyochangia kuondoka kwake Manchester United.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 37 alifungulia Ureno ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 65 baada ya kuchezewa visivyo na beki Mohammed Salisu wa Southampton ndani ya kijisanduku.

Awali, Ronaldo aliyekuwa akivalia utepe wa nahodha alipoteza nafasi nyingi za kumwacha hoi kipa wa Ghana, Lawrence Ati-Zigi. Japo Ronaldo alifunga goli katika kipindi cha kwanza, bao hilo halikuhesabiwa baada ya kubainika kwamba alikuwa amemsukuma Alexander Djiku.

Ghana waliimarisha mchezo wao katika kipindi cha pili baada ya fowadi Mohammed Kudus kuchangia bao lililojazwa kimiani na Andre Ayew katika dakika ya 73.

Hata hivyo, Ureno walijibu pigo hilo kwa mabao mawili ya haraka yaliyopachikwa wavuni na Joao Felix na Rafael Leo chini ya dakika mbili. Osman Bukari alifunga bao la pili la Ghana waliopoteza nafasi ya kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Inaki Williams aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya kipa Diogo Costa.

Ushindi wa Ureno uliwakweza kileleni mwa Kundi H ikizingatiwa kwamba Uruguay na Korea Kusini waliambulia sare tasa katika pambano la awali ugani Education City.

Bao la Ronaldo lilikuwa lake la 118 kimataifa. Manane kati ya mabao hayo yametokana na mechi za hatua ya makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Mabao kutoka kwa Bukari na Ayew ambaye ni fowadi wa zamani wa West Ham United na Swansea City yaliendeleza rekodi ya Ghana kufunga katika mechi sita zilizopita za Kombe la Dunia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay na Korea Kusini watoshana...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nyota Breel Embolo aongoza Uswisi...

T L