• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:03 PM
Tundo, Carol Radull wapata kazi Safari Rally, Talanta Hela mtawalia

Tundo, Carol Radull wapata kazi Safari Rally, Talanta Hela mtawalia

AYUMBA AYODI Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Ababu Namwamba ameteua dereva Carl Tundo na mwanahabari Carol Radul kuendesha miradi ya Mbio za Magari za Dunia (WRC) Safari Rally na Baraza la Talanta Hela, mtawalia.

Katika notisi ya gazeti rasmi la serikali iliyotolewa Ijumaa, Namwamba alisema kuwa wajumbe wa kamati ya uendeshaji na kuandaa Safari Rally watahudumu kwa mwaka mmoja kutoka Januari 4, 2022. Safari Rally itakuwa duru ya saba kati ya 13 za WRC 2023. Itaandaliwa Juni 22-25 katika kaunti ya Nairobi na Nakuru. Namwamba ni mwenyekiti wa kamati ya uendeshaji ya Safari Rally akisaidiwa na Katibu katika Wizara ya Michezo Jonathan Mueke. Mwenyekiti wa Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF) Phineas Kimathi ni katibu katika kamati hiyo ambayo pia ina katibu wa masuala ya vijana na sanaa Ismail Madey, mkurugenzi wa KMSF Surinder Thatthi na afisa mkuu mtendaji wa benki ya KCB, Paul Russo.

Wizara za Utalii, Mambo ya Misitu na Wanyamapori na Urithi na Baraza la Magavana pia zitawakilishwa katika kamati ya uendeshaji Safari Rally. Bingwa mara tano wa Safari Rally, Tundo atasaidiwa na Brian Mutembei. Maafisa wengine ni Hellen Shiri, Jagjett Patter, Kimathi, Hudson Ojiambo, Antony Wanjohi Kanyi, Kiki Christopher, Robert Onyonka, Nyatichi Nyasani, Muema Muindi, Gurdeep Singh Panesar na Dennis Mondet.

Radul atasimamia kamati ya uendeshaji ya Talanta Hela iliyo na wanakamati 10 wanamichezo watajika Julius Yego, Boniface Ambani na Sammy Shollei pamoja na Collins Kale, Kevin Mutai, Alfred Makotsi, Shilovelo Winna Shilavula, Daniel Nakeor na Staicy Ochieng’.

Kamati hii itahudumu kwa miaka mitatu. Majukumu yake ni pamoja na kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo ikiwemo kuweka juhudi za kusaidia timu ya taifa ya soka ya Harambee Starlets (wanawake) na Harambee Stars (wanaume) kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2027 na 2030, mtawalia.

Kamati ya Radull pia itafanya mikakati inayolenga kuimarisha idadi ya medali za katika michezo ya Olimpiki 2024 mjini Paris na 2028 mjini Los Angeles.

Itasaidia Akademia ya Kitaifa ya Michezo (KAS) katika kuendesha mradi wa kitaifa wa kutafuta talanta, kukuza na kunadi Kenya kutoka kaunti zote 47. Kamati hiyo pia itaendesha mashindano ya soka ya kila mwaka ya Bottom Under-19 kutoka mashinani ambayo kilele kitakuwa siku ya Jamhuri Dei hapo Desemba 12.

Isitoshe, kamati ya Radull pia itabuni mfumo utakaofanikisha Kenya kuwa chaguo la kitalii la wanamichezo chini ya mradi wa ‘SportSafari’.

Namwamba atakuwa mwenyekiti wa Baraza la Talanta Hela litakalokuwa na Mueke na Madey kama wanakamati pamoja na Katibu wa Elimu Kisito Wangalwa na mwakilishi kutoka Baraza la Magavana.

June Chepkemei, ambaye majuzi aliteuliwa kuwa kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la uwekezaji nchini Kenya (KenInvest), Dennis Itumbi, David Langat, Debra Mallowah, Abraham Kipyego Mutai, Charles Gacheru, Claudia Naisabwa Leshomoo na Nobert Ouma pia ni wanakamati wa Talanta Hela.

  • Tags

You can share this post!

Olivier Giroud abeba AC Milan dhidi ya Torino katika Ligi...

PENZI LA KIJANJA: Anaweza kukwama kwako na hakupendi

T L