• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:50 AM
Uholanzi wapepeta Ubelgiji katika Uefa Nations League

Uholanzi wapepeta Ubelgiji katika Uefa Nations League

Na MASHIRIKA

UHOLANZI walianza kampeni zao za Uefa Nations League mnamo Ijumaa kwa ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Ubelgiji walioshuhudia fowadi matata Romelu Lukaku akipata jeraha baya litakalomweka nje kwa muda mrefu.

Mshambuliaji Memphis Depay wa Barcelona alipachika wavuni mabao mawili ya Uholanzi katika gozi hilo lililotandaziwa jijini Brussels. Magoli mengine ya Uholanzi yalijazwa kimiani kupitia Steven Bergwijn wa Tottenham Hotspur na Denzel Dumfries wa Inter Milan.

Ubelgiji waliopoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Timothy Castagne na Dries Mertens, walifutiwa machozi na Michy Batshuayi.

Ushindi wa Uholanzi uliendeza rekodi ya kutopigwa kwa kikosi hicho chini ya kocha mpya Louis van Gaal kutokana na mechi 10 zilizopita.

Kikosi hicho kimezidi kujisuka upya na kupata uthabiti mkubwa tangu kiliposhindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi na kudenguliwa mapema katika hatua ya nane-bora kwanye fainali za Euro 2020.

Uholanzi waliteremkia wenyeji wao kwa urahisi katika pambano hilo la Kundi A4 baada ya Lukaku kuumia alipokabiliana na beki Nathan Ake. Sogora huyo wa zamani wa Everton na Manchester United amekuwa na msimu wa kutoridhisha kambini mwa Chelsea aliowafungia mabao 15 pekee tangu aagane na Inter Milan mwishoni mwa 2020-21.

Ubelgiji wanatarajiwa sasa kujinyanyua ugenini dhidi ya Wales mnamo Juni 8, 2022 huku Uholanzi wakialika Poland kwa pambano jingine la Kundi A4.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sampuli za wanaohofiwa kuugua ‘monkeypox’ kupimwa...

Kiti moto cha useneta Mombasa chavutia 14

T L