• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 10:50 AM
Ushindani mkali kushuhudiwa mechi za KWPL

Ushindani mkali kushuhudiwa mechi za KWPL

Na JOHN KIMWERE

KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye kampeni za mechi za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka la Wanawake (KWPL) msimu huu.

Gaspo Women ya kocha, Domitila Wangui jumamosi hii itashuka ugani Stima Club, Nairobi kuvaana na mabingwa watetezi, Thika Queens.  ”Tunatarajia mtihani mgumu mbele ya wageni wetu ilhali tuna majeraha kadhaa ambapo tutakosa huduma za wachezaji wetu tegemeo akiwamo Bertha Omita kati ya wengine,” kocha huyo alisema na kutoa wito kwa warembo wake watakaoshiriki kujiamini wanaweza na kujituma bila kulegeza kamba.

Naye meneja wa Thika Queens, Glenston Muganda anasema ”Tutakuwa kazini kuwinda ushindi wa alama zote muhimu ili kujiongezea tumaini la kutimiza azma yetu muhula huu.”

Nayo Kangemi Allstars ya kocha, Joseph Orao bado Jumamosi hii itakaribisha Kisumu Allstarlets katika uga wa Stima Club. ”Tunavuta mkia lakini tunaamini tuna uwezo wa kutikisa nyavu. Lazima tujikaze kiume ili kujinasua kutoka mduara wa kushushwa ngazi,” kocha Orao alisema na kutaka mabeki wake kutoruhusu kufungwa mabao ya ovyo.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Zetech Sparks ya kocha, Benard Kitolo itachuana na Kayole Starlets. Zetech itacheza mchezo huo huku ikijivunia kutandika Kisumu Allstarlets mabao 3-1 wiki iliyopita.

Wachezaji wa Ulinzi Starlets wakisherekea baada ya kufunga bao kwenye mechi ya Ligi Kuu…Picha/JOHN KIMWERE

Nao vipusa wa Maafande wa Ulinzi Starlets wa kocha, Joseph Wambua Mwanza watakuwa Ruaraka kuialika Wadadia FC, mabingwa wa zamani Vihiga Queens watazuru mjini Kitale kupepetana na Trans Nzoia Falcons huku Nakuru City Queens ikikaribisha Bunyore Starlets.

Kwenye msimamo wa kipute hicho, Vihiga Queens inaongoza kwa kusajili alama 35. Nayo Gaspo inashikilia nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 28, mbili mbele ya Ulinzi Starlets sawa na Thika Queens tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Wchezaji wa Gaspo Women wasikiza mawaidha ya makocha wao…Picha/JOHN KIMWERE

 

You can share this post!

Frankfurt kukutana na West Ham kwenye nusu-fainali ya...

Fortune yapania kusajili watatu

T L