• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Watu 4 wa familia moja waangamia ajalini

Watu 4 wa familia moja waangamia ajalini

NA RICHARD MAOSI

FAMILIA ya watu wanne walioangamia , asubuhi ya Jumapili karibu na Two Rivers Mall kaunti ya Kiambu, walikuwa wakisafiri kutoka Arahuka iliyoko kaunti ya Nakuru, kuelekea Nairobi.

Katika ajali hiyo Bw Peter Miano mwenye umri wa miaka 35, ndiye alikuwa ameshika usukani, alipogongana ana kwa ana na gari jingine, ambalo kulingana na Ripoti ya Polisi lilikuwa likiendeshwa kwa kasi.

Mkewe Susan Wahome na watoto wao wawili, Everlyn Wahome na Prince Wahome pia waliangamia kutokana na majeraha mabaya.

Taifa Leo Dijitali ilitembelea nyumbani kwa akina Miano, siku ya Jumanne katika eneo la Bahati, kaunti ya Nakuru ambapo shughuli za mazishi zilikuwa zikiendelea.

Wahome Gichuki ambaye ni babake marehemu anasema alipata taarifa hizo za huzuni siku ya Jumapili mwendo wa saa kumi alasiri hivi baada ya kutoka kanisani.

Wahome anasema kuwa mwanawe alikuwa akipenda sana michezo hususan kandanda na ule wa kututumua misuli.

“Ingawa bado alikuwa na familia changa,nitamkumbuka kwa bidii zake na jinsi alikuwa mtu wa watu,”akasema.

Wahome aliongezea kuwa mwanawe alikuwa ameweka mipango ya kuwatambulisha wazazi wake kwa familia ya akina mkewe msimu wa Pasaka 2021.

Aidha kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia na jamii, ikizingatiwa kuwa alikuwa ni mfanyibiashara na alikuwa tegemeo nyumbani.

Miili yao imehifadhiwa katika eneo la Freearea ambapo watazikwa wiki ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Timu ya Viziwi Nakuru yajiandaa kwa mashindano ya Afrika

Umetuvunjia heshima, wasusi wamfokea Boniface Mwangi