• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:08 PM
Achani akemea washindani wanaodharau wagombeaji wa kike

Achani akemea washindani wanaodharau wagombeaji wa kike

NA SIAGO CECE

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bi Fatuma Achani, amekosoa wapinzani wake anaodai kuwa wanamdhalilisha kwa sababu ya jinsia yake wanapotafuta kura za uchaguzi wa ugavana katika kaunti hiyo.

Bi Achani, ambaye ndiye mwaniaji pekee wa kike wa ugavana katika Kaunti ya Kwale, aliwataka wakazi kutowapa sikio wanaojitafutia sifa kwa kumdunisha kama kiongozi mwanamke.

“Wanaponizungumzia vibaya wanawadhalilisha wanawake wote. Wakazi hawapaswi kuwasikiliza viongozi wanaopanda jukwaani na kuzungumza vibaya kuhusu wagombeaji wa kike. Viongozi wanapaswa kuzungumzia na kuuza sera zao,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika eneo la Matuga baada ya kuidhinishwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC) jana kuwania kumrithi Gavana Salim Mvurya.

“Ikiwa watakuwa wanatembea wakinidhalilisha mimi kama mama, Wakwale itabidi wakatae siasa hiyo,” Bi Achani akasema.

Bi Achani alisema kuwania kiti hicho kama mwanamke pekee ni mwanzo mpya wa kisiasa katika Kaunti. Alieleza kuwa licha ya chamngamoto anazopitia, ataendelea kuwania kiti hicho na kuwa mfano bora kwa wanawake wengine.

Alisema uongozi wake ni hatua nzuri katika kuhakikisha kuwa nchi inakidhi matakwa yake ya kikatiba ambayo yanawapa wanawake nafasi ya kuongoza.

Bi Achani amekuwa naibu gavana wa Kwale kwa miaka 10 baada ya kuchaguliwa mwaka wa 2013 kama mgombea mwenza wa Gavana Mvurya.

Anawania chini ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) baada ya kupewa tikiti ya moja kwa moja na chama hicho kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Gavana Mvurya aliye katika muhula wake wa mwisho amemwidhinisha Bi Achani kuwa mrithi wake akisema ana uwezo wa kutosha kuongoza

“Hatukuwa kama magavana wengine ambao walikuwa na manaibu wao tu kama picha. Nilimshirikisha Bi Achani katika maamuzi yote muhimu akiwa naibu na kumpa majukumu ya uongozi na nina imani naye, ndiyo maana ninataka kumwachia uongozi,” akasema Bw Mvurya.

Aliongeza kuwa jinsia ya Bi Achani haipaswi kutumiwa kama kikwazo kwa kampeni zake, na kuongeza kuwa wataendelea kufanya kazi pamoja.

“Kwa wale ambao hawajaamini katika uongozi wa nawake, wanapaswa kumpa Bi Achani nafasi ili wajionee,” alisema. Washindani wa Bi Achani ni Prof Hamadi Boga (ODM), Chai Lung’anzi (PAA), Gereza Dena (Kanu), Sammy Ruwa (Huru) na Chirau Ali Mwakwere (Wiper).

Prof Boga na Bw Mwakwere tayari wameidhinishwa na IEBC huku Bw Dena, Bw Lung’anzi na Bw Ruwa wakisubiri zoezi hilo Jumatatu.

Kwa sasa Bw Mvurya ni mmoja wa vinara wakuu wa Kenya Kwanza baada ya Dkt Ruto kuahidi kuwa atamteua kuwa mmoja wa viongozi wa kitaifa iwapo serikali yake itashinda.

  • Tags

You can share this post!

11 wafa ajalini Kitui wakitoka hafla ya kulipa mahari

Nassir kupigwa jeki akiidhinishwa na IEBC kwa ugavana

T L