• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Nassir kupigwa jeki akiidhinishwa na IEBC kwa ugavana

Nassir kupigwa jeki akiidhinishwa na IEBC kwa ugavana

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, atapigwa jeki katika uwaniaji wa ugavana wa Mombasa ikiwa ataidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mpinzani wake wa karibu, Bw Mike Sonko, alizimwa na IEBC mnamo Jumamosi huku wawaniaji wengine watatu ‘wakirudishwa nyumbani’ jana kwa kupatikana na makosa wanayofaa kurekebisha.

Wakati uo huo, IEBC ilisema aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar, wa chama cha UDA aliomba muda zaidi huku Bw Anthony Chitavi (UDP), pia akizimwa kuwania.

Kuingia kwa Bw Sonko dakika za mwisho katika kinyang’anyiro hicho cha kumrithi Gavana Hassan Joho, kulikuwa kumehatarisha uwezo wa Bw Nassir kuzoa kura nyingi kwa mteremko ifikapo Agosti 9, kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanywa na mashirika mbalimbali ya utafiti.

Kura ya maoni iliyokuwa imedhaminiwa na kampuni ya Nation Media Group ilikuwa imeonyesha kwamba Bw Nassir angemshinda Bw Sonko kwa asilimia saba pekee za kura endapo uchaguzi ungefanywa mwezi uliopita.

Mbali na Bw Sonko kuvutia wapigakura wengi kwa aina yake ya siasa, hasa za kulenga utoaji misaada vitongojini, wadadisi walikuwa wameonya kuwa angemvuruga Bw Nassir maadamu vyama vyao vya Wiper na ODM ni washirika katika chama cha muungano cha Azimio la Umoja-One Kenya.

Kwa msingi huo, ilitarajiwa wafuasi wa mgombeaji urais wa Azimio, Bw Raila Odinga, wangegawanya kura za ugavana katika kaunti hiyo.

Nyota ya Bw Sonko ilizimwa Jumamosi pale mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, alipotangaza uamuzi kwamba viongozi waliong’atuliwa mamlakani kwa sababu za kimaadili hawastahili kisheria kushikilia wadhifa wowote serikalini.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nassir alisema uamuzi wa IEBC haukuwa wa kisiasa kwa kuwa tume hiyo ni huru na pamoja na hayo, sheria ilifuatwa.

“Si kazi yangu kutathmini hati za watu. Mimi sishindani na mtu yeyote. Ninashindana dhidi yangu binafsi nikilenga azma yangu ya kushinda uchaguzini Agosti 9,” akasema.

Wiki iliyopita, IEBC iliorodhesha majina tisa ya wawaniaji wa kumrithi Gavana Joho. Wengine walioorodheshwa ni Bw Daniel Kitsao (mgombea huru), Bw Shafii Makazi (UPIA), Bw Said Abdalla (Usawa kwa Wote), Bw Hezron Awiti (VDP), na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi (PAA).

Mabw Awiti na Kitsao walirudishwa nyumbani jana baada ya stakabadhi zao kupatikana kuwa na doa huku Dkt Kingi akikosa kupewa cheti baada ya mgombea mwenza wake, Bw Amin Roble, kutakiwa arekebishe stakabadhi zake.

“Tumewaongeza muda warekebishe makosa yaliyobainika,” alisema msimamizi wa IEBC katika Kaunti ya Mombasa, Bi Swalhah Yusuf.

Kuondolewa kwa Bw Sonko, kumemwacha mgombea mwenza wake, Bw Ali Mbogo katika njiapanda.

Awali Wiper ilisema ina mpango mbadala endapo Bw Sonko hangeruhusiwa kuwania. Hata hivyo, kufikia jana, Wiper haikuwa imebainisha hatua itakayochukuliwa.

Bw Sonko alilalamikia hatua ya IEBC dhidi yake akidai ni ukiukaji wa sheria, kwa vile alikata rufaa katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa kubanduliwa mamlakani Nairobi.

Vile vile, jopo la majaji walioteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome, bado linasubiriwa kutoa uamuzi kuhusu kama wanasiasa wanaong’atuliwa vitini kwa sababu za kimaadili wanastahili kuwania viti au la.

  • Tags

You can share this post!

Achani akemea washindani wanaodharau wagombeaji wa kike

Kingi afichua siri ya kuungana na Ruto kwa uchaguzi

T L