• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Hofu pesa za wizi zinapaka tope uchaguzi

Hofu pesa za wizi zinapaka tope uchaguzi

NA COLLINS OMULLO

MASHIRIKA ya kijamii nchini, yamesema kwamba kuna hatari ya mabilioni ya pesa haramu kutumiwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ujao kutokana na ukosefu wa sheria ya kudhibiti kiwango cha pesa ambazo wawaniaji wanapaswa kutumia kujipigia debe.

Wakizungumza na wanahabari jijini Nairobi, viongozi wa mashirika hayo wanasema kwamba matumizi ya pesa zilizopatikana kwa njia isiyo ya kisheria, yanaweza kupaka tope uchaguzi kwa kuinua utoaji hongo.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Mzalendo Trust, Caroline Gaita, matumizi ya pesa haramu yanavuruga misingi ya demokrasia.

Bi Gaita alisema kwamba uchaguzi mkuu wa Agosti 9 utakuwa wa tatu kufanyika Kenya bila pesa ambazo wanasiasa watatumia kudhibitiwa.

“Pesa ni moja ya vigezo vinavyoamua hali ya uchaguzi mkuu wa nchi yoyote,” alisema.

Wiki jana, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitilia shaka vyanzo va pesa ambazo baadhi ya wanasiasa wanatumia katika kampeni na akaonya kuwa walanguzi wa pesa wanatishia uadilifu wa Uchaguzi Mkuu ujao.

Bw Matiang’i alieleza hofu yake kwamba wahalifu wanaweza kutumia pesa chafu kuhongana ili waingie ofisini.

“Uchaguzi nchini Kenya ni wa tatu katika zile ghali ulimwenguni. Pesa zinatupatia viongozi walio na maswali ya kimaadili kwa hivyo ni muhimu pesa za kampeni ziweze kudhibitiwa,” alisema Bi Gaita.

Alisema wanasiasa wanapotumia mabilioni ya pesa bila kudhibitiwa, makundi ya vijana, wanawake na watu walio na ulemavu hayawezi kupata nafasi ya kuingia uongozini.

“Pesa zinazotumiwa katika uchaguzi zikikosa kudhibitiwa, vijana, wanawake na watu walio na ulemavu huwa wanabaguliwa kwa kuwa hawawezi kushindana na pesa za kutiliwa shaka za baadhi ya wawaniaji,” akasema.

Mwanaharakati huyo alitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuweka kanuni za kudhibiti pesa zinazotumiwa katika uchaguzi na kuzichapisha.

“Tunahimzia serikali kutuimia habari zozote za ujasusi inazopata kuhakikisha kuwa wale wanaohusika na ulanguzi wa pesa na vitendo vya uhalifu wanakamatwa. Tusiruhusu wahalifu kuteka nyara mchakato wetu wa uchaguzi na kufungia raia wanaofuata sheria ambao wanaweza kuleta mageuzi yanayohitajika katika uongozi,” akasema.

Mkurugenzi Mkuu wa Transparency International-Kenya Sheila Masinde alisema kuna wawaniaji kadhaa ambao maadili yao ni ya kutiliwa shaka, ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na vitendo vya uhalifu, wengine wana kesi zinazoendelea kortini na walioondolewa ofisini kupitia miswada ya kuwatimua, lakini wameidhinishwa na vyama vyao kuwania viti kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Alisema ili kulinda uadilifu wa uchaguzi Kenya, watu ambao maadili yao yanatiliwa shaka hawafai kuwania viti kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Kuna wale walio na kesi zilizo wazi kama vyeti feki za masomo na asasi husika zimethibitisha, baadhi wamehusika kwenye ghasia na matamshi ya chuki na uchochezi,” alisema.

Naye mkurugenzi wa Taasisi ya Sheria ya Uchaguzi na Utawala Afrika

Felix Owuor alisema viongozi waliotimuliwa ofisini hawafai kugombea viti kwa sababu maadili yao ni ya kutiliwa shaka.

Naye mshirikishi wa kitaifa wa Elections Observation Group (ELOG) Mulle Musau alisema kulinda uadilifu wa mchakato wa uchaguzi ni muhimu ili kuhakikisha utakuwa wa amani huru na wa kuaminika.

  • Tags

You can share this post!

Uzalishaji wa mahindi, maharagwe na ngano washuka, bei...

TUSIJE TUKASAHAU: Wapi Baraza la Kiswahili la Kenya?

T L