• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Jalang’o ashinda tiketi ya ODM kuwania kiti cha ubunge Lang’ata

Jalang’o ashinda tiketi ya ODM kuwania kiti cha ubunge Lang’ata

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA mtangazaji wa redio Jalang’o Phelix Odiwuor sasa ndiye atapeperusha bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha ubunge Lang’ata katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Jalang’o ambaye pia ni msanii katika tasnia ya ucheshi, alishinda kwa kupata kura 3,509 dhidi ya mshindani wake wa karibu Oscar Omoke aliyepata kura 1,612 katika mchujo huo uliofanyika Ijumaa, Aprili 22, 2022.

Musari Kahiga Syongoh alishika nambari ya tatu kwa kupata kura 397 huku Wangusi Nathan Barasa akiwa wa nne kwa kupata kura 146.

Katibu mpanga ratiba wa klabu ya Gor Mahia Sally Bolo alikuwa wa tano kwa kujishindia kura 138 huku Taa Vivienne akiwa wa mwisho kwa kupata kura 121 pekee.

Bw Jalang’o sasa atakabiliwa na Mbunge wa sasa wa Langata Nixon Korir wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mkuu.

Katika eneobunge la Westlands mwanawe aliyekuwa mbunge wa hapo, Fred Gumo, Michael Magema Gumo, alimshinda Philip Kisia kwa kupata kura 1,661.

Kisia ambaye zamani alikuwa Karani wa lililokuwa Baraza la Jiji la Nairobi, alipata kura 627 katika kinyang’anyiro hicho cha kusaka tiketi ya ODM kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu.

Kura hiyo ya mchujo iliendelea Ijumaa hiyo licha ya chama cha ODM kutangaza kusitishwa kwake kufuatia kurejea kwa Tim Wanyonyi katika kinyang’anyiro cha kutetea kiti hicho kwa muhula wa tatu.

Hii ni baada ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kumshinikiza Bw Wanyonyi kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi.

Mbunge huyo alishauriwa ampishe Bw Polycarp Igathe ambaye aliteuliwa na chama tawala cha Jubilee kuwania kiti hicho.

  • Tags

You can share this post!

Waislamu Mlima Kenya watoa wito Wakenya wadumishe upendo na...

Kiwango cha uzalishaji nyama ya ng’ombe kimeshuka nchini...

T L