• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Jamleck Kamau kupeperusha bendera ya Jubilee ugavana Murang’a

Jamleck Kamau kupeperusha bendera ya Jubilee ugavana Murang’a

NA GATUNI WACHIRA

CHAMA cha Jubilee kimempa mwaniaji wa ugavana katika Kaunti ya Murang’a Jamleck Kamau tiketi ya moja kwa moja.

Hii ni licha ya chama hicho kukejeliwa kwamba kimekosa maana hasa baada ya wanachama wengi kukihama na kujiunga na chama cha Naibu Rais William Ruto cha United Democratic Aliance (UDA).

Akizungumza na wakazi wa Muthithi, Murang’a, Bw Kamau alisema kwamba alikuwa tayari kutumia chama hicho kama daraja la kumfikisha kilele cha uongozi wa Kaunti ya Murang’a, baada ya gavana wa sasa Mwangi wa Iria kumaliza mihula yake miwili .

“Nimeona ni vyema kutumia daraja la Jubilee ili nipate nafasi ya kutwaa uongozi wa Kaunti hii ya Murang’a. Nyote mnajua vizuri pale tulipo, nawaomba sana mniunge mkono, bila kubagua chochote ili  niyajali maslahi yenu wenyewe,” alisema.

Bw Kamau alisema kwamba alifikia hatua hiyo baada ya kufanya mashauriano na washikadau katika wadi zote katika Kaunti ya Murang’a ambako kulingana naye, ushauri ulikuwa ni kupata tiketi ya chama cha Jubilee katika kuwania wadhifa wa ugavana katika uchaguzi ujao.

Mbunge huyo wa zamani wa Kigumo, alisema kwamba yuko tayari kushirikiana na serikali yoyote ambayo itachaguliwa mnamo mwezi Agosti akisema kwamba haja yake ni watu wa Murang’a kupata mgao wao wa serikali ya Kaunti.

Bw Kamau ambaye anatambulika sana kutokana na usemi wake mkubwa katika Mlima Kenya, aliwaeleza wakazi wa Murang’a kwamba hana haja na watakayempigia kura za urais.

“Mimi namwambia wananchi wa Murang’a kwamba pana serikali mbili: Serikali ya Kitaifa na Serikali ya Kaunti ya Murang’a. Mimi sina usemi wa ni nani mtakayemchagua kama rais, haja yangu ni ugavana,” akasema.

Bw Jamleck Kamau kadhalika alifichua kwamba chama cha Jubilee hakitafanya uchaguzi wa mchunjo wa Ugavana katika Kaunti ya Murang’a kwa kuwa hakina wawaniaji wengine kwa tiketi ya chama hicho.

Hii itakuwa mara ya pili Bw Kamau kuwania ugavana baada ya kuwania wadhifa huo huo na kuibuka wa pili katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa wa 2017. Aliposhidwa katika uchaguzi huo aliamua kupiga breki siasa na kuchapa kazi kwingineko.

Mapema mwaka jana, aliwaarifu vijana kwamba alipiga breki siasa ili kumpa nafasi nzuri Gavana wa sasa Mwangi Wa Iria kumaliza muhula wake wa pili, akiahidi kuhakikisha kumalizika kwa miradi aliyoianzisha Wa Iria.

Kati ya miradi aliyoapa kumaliza ni mradi wa ng’ombe wa maziwa, ambapo wakulima wa Murang’a  hupokea shillingi 35 kwa kila lita ya maziwa, hatua ambayo imewezeshwa na Serikali ya Kaunti kupitia kwa kiwanda cha maziwa ambacho huzalisha zaidi ya lita 100,000 za maziwa kila siku.

Kamau ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Maendeleo ya Tana na Athi River pia aliahidi kuanzisha viwanda ambavyo vitatumia bidhaa asili za eneo hilo kama ndizi na maparachichi ili kuwaepusha wakazi umaskini.

  • Tags

You can share this post!

Mapenzi kwao basi!

Kalonzo atoa masharti mapya kusalia Azimio

T L