• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Kalonzo atoa masharti mapya kusalia Azimio

Kalonzo atoa masharti mapya kusalia Azimio

NA PIUS MAUNDU

WIKI moja baada ya Kalonzo Musyoka kuunga mkono azma ya urais ya kiongozi wa ODM Raila Odinga,kinara huyo wa Wiper Democratic Movement amedokeza kuwa huenda akabadili msimamo huo.

Hii ni baada ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na wasimamizi wa kampeni za Bw Odinga kushikilia kuwa, Wiper ilijiunga na Azimio la Umoja kama chama binafsi na wala sio kama mshirika wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Bw Musyoka alisema yeye ni miongoni mwa viongozi watatu wenye usemi mkuu katika muungano wa Azimio-OKA, mwingine akiwa Rais Uhuru Kenyatta anayewakilisha chama cha Jubilee.

Alimtaka Bw Odinga na Rais Kenyatta kuongozwa na mchakato uliokwama wa marekebisho ya Katiba, ili kuonyesha waziwazi kile ambacho yeye (Kalonzo) atapata katika serikali ya Bw Odinga. Alifichua kuwa anata – ka wadhifa wa Naibu Rais katika serikali ya Bw Odinga.

Hata hivyo, alisema yu tayari kukubali wadhifa mwingine mkuu katika serikali hiyo, mradi Bw Odinga ahakikishie jamii ya Wakamba kuwa itapata thuluthi tatu ya nyadhifa zote za uongozi katika serikali yake.

Bw Musyoka alitishia kujiondoa kutoka kwa muungano huo mkuu endapo thamani yake “itahujumiwa”.

“Kama OKA, tutakuwa kinyang’anyironi kwa sababu tumebuni mkataba wa makubaliano wenye umbo la kiti chenye miguu mitatu kijulikanacho kama Azimio-One Kenya Alliance.

“Mazungumzo kuhusu ugavi wa mamlaka yakianza, mtanisikia nikisisitiza kuwa sharti tutengewe thuluthi moja ya nyadhifa zote serikali, ili tusisalitiwe tena,” Bw Musyoka akasema jana kwenye mahojiano katika kituo cha redio cha Musyi FM, inayopeperusha matangazo kwa lugha ya Kikamba.

Alalamika kabla ya kutiwa saini kwa mkataba wa muungano wa Azimio la Umoja, wikendi iliyopita, Rais Kenyatta na Bw Odinga walimkalisha katika Ikulu ya Nairobi kwa zaidi ya saa tatu.

Alimsawiri Bw Odinga kama kiongozi ambaye hupenda kuwasaliti wenzake huku akiwalaumu magavana watatu wa Ukambani kwa kumhujumu ili asiteuliwe kuwa mgombeaji mwenza wa kiongozi huyo wa ODM.

Uhasama wa muda mrefu kati ya Bw Musyoka na magavana Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni) umetisha kuvuruga kampeni za Bw Odinga katika eneo la Ukambani.

Bw Musyoka alisema katu hatafanya mikutano ya pamoja na magavana hao kuvumisha Bw Odinga, akisisitiza kuwa yeye ndiye kigogo wa Ukambani. “Odinga atakapozuru Ukambani, tutaondoka na kuelekea Kisumu na maeneo mengine ya nchi kumfanyia kampeni ili kutoa nafasi akaribishwe na magavana hao,” akasema.

Bw Musyoka alisema kuwa anamtegemea Rais Kenyatta kuhakiksha kuwa Bw Odinga hamsaliti kwa mara nyingine.

“Huku tukimuunga mkono Raila, tunatumai kuwa wanalipa sehemu ya mwisho ya mgao wa fedha za hazina ya ustawi wa vyama. Historia inaonyesha kuwa wingu la kutoaaminiana limegubika mahusiano kati yangu na Bw Odinga tangu enzi za LDP, NARC, CORD na NASA. Hii ndio maana ninakubali kwamba mtu asiyependelea upande wowote kama vile kiongozi wa chama cha Jubilee kusimama kati yetu ili kupoesha jo – to,” akaeleza.

Bw Musyoka alipendekeza kuwa kuandaliwe vikao vingi vya mazungumzo kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ili kupunguza uwezekano wa Bw Odinga kumsaliti tena. Hayo yanajiri huku vyama zaidi ya 20 vilivyomo ndani ya Azimio la Umoja wakiwa vikitaka kuona yaliyomo kwenye mkataba uliotiwa saini wikendi iliyopita.

Katibu Mkuu wa Wiper Shakila Abdalla amefichua kuwa yeye na maka – tibu wenzake waliambiwa kutia saini katika ukurasa wa mwisho lakini hawakusoma yaliyomo.

Bw Kalonzo amekuwa akisema kuwa alitia saini makubaliano ya kutaka muungano huo kuitwa Azimio-One Kenya – kauli ambayo imekosolewa vikali na wanasiasa wa ODM.

“Muungano mkubwa utakaosajiliwa katika Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa utajulikana kama Azimio One Kenya,” akasema Bw Musyoka.

Tangu kutia saini mkataba wa kujiunga na Azimio la Umoja, Bw Musyoka amekuwa akitoa kauli za kukanganya wafuasi wake. Hivi majuzi alisema kuwa ataanza kampeni zake za urais za Uchaguzi Mkuu wa 2027 mara tu baada ya Bw Odinga kuapishwa.

  • Tags

You can share this post!

Jamleck Kamau kupeperusha bendera ya Jubilee ugavana...

Njaa kuumiza Wakenya zaidi 

T L