• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Junet, Babu wadadisiwa na DCI

Junet, Babu wadadisiwa na DCI

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Suna Mashariki Junet Mohamed alijiwasilisha katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumanne, Aprili 5, 2022 kutoa maelezo kuhusu kisa ambapo helikopta ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ilipigwa kwa mawe katika kaunti ya Uasin Gishu.

Hii ni baada ya kuagizwa kufika katika afisi hizo zilizoko katika barabara ya Kiambu, Nairobi ili ahojiwe kuhusiana na tukio hilo lililolaaniwa na viongozi wengi, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Mohamed ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa aliwaambia wanahabari, baada ya kuhojiwa na maafisa wa DCI.

“Nimewapa maafisa wa DCI maelezo yote ambayo nadhani yatawasaidia katika uchunguzi wao kuhusu kisa hicho kilichotokea baada ya Raila Odinga kufika katika boma la rafiki yake marehemu Jackson Kibor kufariji familia yake,” akasema.

“Tunatarajia kwamba DCI watafanya uchunguzi wa kina na kufichua ukweli kuhusu tukio hili la aibu,” Bw Mohamed akaeleza.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenyekiti wa ODM John Mbadi pia waliandikisha taarifa mbele ya maafisa hao wa DCI wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi katika asasi hiyo, John Gachomo.

Bw Owino ni miongoni mwa wanasiasa walioandamana na Bw Odinga wakati wa tukio hilo lililotokea hatua chache kutoka kwa boma la Mzee Kibor katika kijiji cha Kibenes katika eneobunge la Soy.

Mnamo Jumapili wabunge Caleb Kositany (Soy), Oscar Sudi (Kapseret) na Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu David Kiplagat walifika katika afisi za DCI, Nakuru ambako walihojiwa kuhusiana na shambulio hilo.

Waliachiliwa huru baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa tano. Hata hivyo, simu zao zilitwaliwa kufanyiwa uchunguzi zaidi. Hii ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa huenda watatu hao walihusika na shambulio hilo.

  • Tags

You can share this post!

Beki chipukizi anayelenga kufikia ubora wa Sergio Ramos wa...

JIJUE DADA: Nini husababisha kina dada kupoteza hamu ya...

T L