• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Karua apaa Kalonzo akifunganya virago

Karua apaa Kalonzo akifunganya virago

LEONARD ONYANGO NA COLLINS OMULO

ILIKUWA siku ya vifijo na nderemo kote nchini wafuasi wa Muungano wa Azimio wakishangilia kuteuliwa kwa Kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua kuwa mwaniaji mwenza wa Raila Odinga kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Hata hivyo, hatua hiyo ilimfanya Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kutangaza kujiondoa kwenye Azimio ili kuwania urais kivyake, ambapo pia alimteua mwanasiasa kutoka Kaunti ya Narok, Andrew Sunkuli kuwa mgombea mwenza wake.

Katika kuchukua hatua hiyo, Bw Musyoka alimpuuza Rais Uhuru Kenyatta ambaye wikendi alitumia kila aina ya mbinu kumshawishi abaki katika muungano huo, na hata kumuahidi cheo cha Mkuu wa Mawaziri iwapo Bw Odinga atashinda urais.

Hata hivyo, Bw Musyoka alishikilia kwa dhati msimamo wake wa awali kuwa hatakubali cheo kingine katika Azimio isipokuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga, ndiposa iliposhindikana akaamua kwenda kivyake.

Taifa Leo iliweza kupata habari za juhudi ambazo Rais Kenyatta aliweka tangu Jumapili kumshawishi Bw Musyoka zikiwemo kukutana Ikulu lakini kinara huyo wa Wiper akakaa ngumu.

Hata juhudi za Bw Odinga kumtembelea Bw Musyoka nyumbani kwake Karen kumbebeleza aendelee kumuunga mkono hazikuzaa matunda.

Ni baada ya Bw Odinga kushidwa ambapo Rais Kenyatta alichukua usukani na kuwaita wawili hao pamoja na Seneta Gideon Moi wa Baringo katika Ikulu, lakini naye pia akagonga mwamba.

Akiwa na matumaini kuwa huenda juhudi zaidi zingeyeyusha moyo wa Bw Musyoka, mnamo Jumapili Bw Odinga alimtembelea tena kigogo huyo wa siasa za Ukambani nyumbani lakini bado akaambulia patupu.

Bw Odinga hakufa moyo na hapo jana aliwatuma marafiki kuzungumza na Bw Musyoka lakini hawakufanikiwa kubadilisha msimamo wake.Bw Musyoka alikiri Bw Odinga alimtembelea akimuomba kuunga mkono chaguo lake la mwaniaji mwenza, Bi Karua.

Seneta Mutula Kilonzo aliashiria kuwa kinara wake alichezewa akidai alikuwa ameahidiwa cheo cha mwaniaji mwenza wa Bw Odinga alipojiunga na Azimio.

Bw Musyoka aliwania urais mnamo 2007 na kuibuka katika nafasi ya tatu baada ya Mwai Kibaki na Bw Odinga.

Mnamo 2013 na 2017 alikuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

“Ni hadi lini Kalonzo atakuwa ndiye tu anaachia wengine? Tumezima azma zetu kwa sababu ya wengine kwa muda mrefu. Tunavyozungumza sasa jina langu limo IEBC kama mwaniaji urais kwa tiketi ya Wiper,” akasema Bw Musyoka.

Alipokuwa akijiunga na Azimio, Bw Musyoka alisema hakuwa na imani na Bw Odinga akidai alikuwa amemsaliti katika ushirikiano wao wa awali.

Bw Kalonzo ndiye mshirika wa tatu katika Azimio kujiondoa baada ya magavana Alfred Mutua (Machakos) wa Maendeleo Chapchap na Amason Kingi (Kilifi) wa Pamoja African Alliance (PAA).

Akimtangaza Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wake, Bw Odinga alimmiminia sifa tele akimtaja kama mtetezi wa haki na kiongozi mwenye msimamo thabiti.

Kulingana na Bw Odinga, Bi Karua aliwabwaga wapinzani wake tisa ambao walifika mbele ya jopo la kuchuja watu waliotaka kuwa wawaniaji wenza wake.

Waliohojiwa na jopo hilo ni Bi Karua, Bw Musyoka, Gavana wa Kitui Charity Ngilu, Mbunge wa Murang’a Sabina Chege na aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.

Wengine ni waziri wa Kilimo Peter Munya, Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa), Lee Kinyanjui (Nakuru) na kiongozi wa chama cha National Liberal Party Stephen Tarus.

Kura ya maoni iliyofadhiliwa na kampuni ya Nation Media Group wiki iliyopita ilionyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya (asilimia 41) walipendelea Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga huku Bw Musyoka akifuatia kwa asilimia 27.

Bw Odinga analenga kutumia uteuzi wa Bi Karua kupenya katika eneo la Mlimani ambapo mpinzani wake mkuu Naibu wa Rais William Ruto ana uungwaji mkono mkubwa.

Kwa uteuzi huo pia ana imani ya kuvutia kura za wanawake kote nchini.Kulingana na mkurugenzi wa uchaguzi wa Jubilee na Mbunge wa Kieni, Kanini Kega, Rais Kenyatta alikuwa akingojea Bw Odinga kutangaza mwaniaji mwenza wake kabla ya kuanza kampeni katika eneo la Mlima Kenya.

“Tumeunda kamati katika kila kituo cha kupigia kura katika eneo la Mlima Kenya. Kamati hizo zinaandaa watu kabla ya Rais Kenyatta kuelekea huko,” akasema Bw Kega.

  • Tags

You can share this post!

Kwa kuteua Karua, Raila alenga kura za wakazi wa Mlima...

Raila ajaribu kumzima Ruto kwa ahadi za vyeo

T L