• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Kingi hafai kumlaumu Raila, asema Mung’aro

Kingi hafai kumlaumu Raila, asema Mung’aro

NA WINNIE ATIENO

MWANIAJI wa Ugavana wa chama cha ODM kaunti ya Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, amemshutumu Gavana Amason Kingi kwa kumlaumu mgombea urais wa muungano wa Azimio Bw Raila Odinga kwa kutotekeleza maendeleo miaka kumi ambayo amekuwa uongozini.

Bw Mung’aro alisema Kilifi imedorora kwa sababu ya uongozi mbaya hasa katika sekta ya afya huku wagonjwa wakilazimika kusaka matibabu katika hospitali za Mombasa.

Bw Mung’aro anashindana na Bw George Kithi (Pamoja African Alliance) na Bi Aisha Jumwa (United Democratic Alliance) ambao wako katika muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Mung’aro alisema Gavana Kingi hafai kumlaumu Bw Odinga kwa kukosa kutekeleza miradi ya maendeleo katika kaunti yake.

“Kama hukufanya kazi, aache kumsingizia Bw Odinga. Umeshindwa na kazi. Hajawahi kunyimwa pesa kwa sababu ya chama, kila mwaka alikuwa akipewa fedha za ugatuzi na seriklai za kitaifa. Lakini sasa anawaambia watu wa Kilifi tatizo ni chama. Tatizo si chama ni uongozi wake mbaya,” alisema Bw Mung’aro.

Bw Kingi anamuunga mkono Bw Kithi huku Naibu wa Rais William Ruto akimpigia debe Bi Jumwa.

Hata hivyo, Bw Mung’aro alisema wapinzani wake hawana ajenda bora kwa wakazi wa Kilifi akiendelea kumshutumu Gavana Kingi kwa kufumbia macho changamoto zinazowakabili wakazi.

“Watu wanalia sababu ya changamoto za maji, ukienda Ganze, Rabai na Kaloleni utasikitika kuona watu wakinywa maji ya mabwawa sawa na ngo’mbe. Kilifi ina shida kubwa sana na mimi tu ndiye nitazitatua kwa sababu nina uzoefu, nimekuwa meya wa Malindi, Mbunge na Waziri Msaidizi,” alisema Bw Mung’aro.

Kadhalika aliwasihi wakazi kumpigia kura Bw Odinga ili Kilifi inufaike na uongozi wa serikali kuu.

Alisema ataendelea kushirikiana na Gavana Hassan Joho ambaye aliteuliwa na Bw Odinga kusimamia kampeni zake pwani kusaka kura.

Gavana Joho amekuwa akipiga kambi Kilifi kuwarai wakazi kumuunga mkono Bw Odinga akisema Pwani itanufaika na uongozi wake.

  • Tags

You can share this post!

Thika Queens kujipanga upya tayari kwa kampeni za msimu

UJAUZITO NA UZAZI: Athari za mimba kuharibika

T L