• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
Kura: Mungatana amtaka Kioni akome kudharau IEBC, mahakama

Kura: Mungatana amtaka Kioni akome kudharau IEBC, mahakama

NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Tana River Danson Mungatana amemshutumu Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni aliyedai kwamba “matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yakionyesha Rais William Ruto alishinda si ya kweli.”

Akiongea na wanahabari mnamo Alhamisi, Januari 19, 2023 katika Majengo ya Bunge, Bw Mungatana amedai Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anadharua asasi ya IEBC na Mahakama ya Juu ambayo ilitumia fedha za umma kuthibitisha kuwa Rais William Ruto ndiye aliibuka mshindi wa kura za urais zilizopigwa Agosti 9, 2022.

Mungatana amesema ni dharau kwa  Bw Kioni kusimama mbele ya Wakenya akiwa na kijikaratasi na kudai amepokea matokeo kutoka kwa mfichuzi asiyejulikana kudharaulia mbali kazi kubwa iliyofanywa na IEBC na Mahakama ya Juu.

Amemshauri Kioni kuhakiki sera za serikali badala ya kutoa matamshi yasiyo na msingi wowote.

“Mheshimiwa Kioni anafaa kukosoa mipango ya serikali na Rais Ruto kuhusu Barabara, Maji, Afya miongoni mwa mambo mengine muhimu kwani hiyo ndio kazi ya upinzani. Akome kutoa madai yasiyo na msingi na ya kudunisha asasi za serikali, ” Bw Mungatana akawaambia wanahabari katika Majengo ya Bunge.

Mnamo Jumatano Bw Kioni alidai kuwa mfichuzi alidokezea muungano wa Azimio eti mgombea wao -Raila Odinga – alipata kura 8,170,355 sawa na asilimia 57.53 ya kura halali za urais zilizopigwa.

Kwenye matokeo rasmi ya IEBC na ambayo yalitangazwa rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti Wafula Chebukati, Rais William Ruto aliibuka mshindi kwa kupata kura 7,176,141 (50.49%) naye mpinzani wake mkuu – Raila – akipata kura 6,942,930 (48.85%).

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: NHIF ifanyiwe mageuzi iwahudumie Wakenya...

Serikali kutumia Sh1.4b kufidia waathiriwa wa mradi wa...

T L