• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Maeneo yatakayoamua wazito kaunti za Pwani

Maeneo yatakayoamua wazito kaunti za Pwani

NA VALENTINE OBARA

WAGOMBEAJI viti vya kisiasa vya eneo la Pwani, wanatarajiwa kuanza kutumia takwimu za wapigakura katika maeneobunge kuweka mikakati kikamilifu kuhusu kampeni zao kabla ya uchaguzi wa Agosti.

Baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kukamilisha awamu ya pili ya kusajili wapigakura wapya, takwimu zinaonyesha maeneobunge ambayo yanatarajiwa kuvutia mapambano makali ya wagombeaji ugavana.

Maeneo haya yanatarajiwa pia kuvutia ushindani mkali wa viti vya useneta na uwakilishi wa wanawake bungeni.

Ingawa IEBC bado inatarajiwa kusafisha takwimu hizo kwa kutathmini wapigakura waliofariki, waliojisajili vibaya na waliohamisha kura zao mbali na kuendeleza usajili vituoni, huenda kusiwe na tofauti kubwa katika orodha ya mwisho itakayotolewa baadaye.

Katika Kaunti ya Mombasa, maeneobunge ya Kisauni, Nyali na Mvita ndiyo yana uwezekano mkubwa wa kuamua mshindi wa viti vya ugavana, useneta na uwakilishi wa wanawake.

Baada ya kukamilika kwa shughuli ya usajili kwa wingi ya wapigakura, wawaniaji wa viti vya ugavana na useneta walenga maeneo yaliyoandikisha usajili wa wapigakura wengi bungeni.

Hii ni kutokana na kuwa, kufikia sasa idadi ya wapigakura waliosajiliwa Kisauni ni 140,299 ikifuatwa na Mvita (125,623) na Nyali (117,241).

Sadfa ni kuwa, mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, mwenzake wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na aliyekuwa mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti ni miongoni mwa wanasiasa wanaotaka kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho.

Katika kampeni zake, Bw Mbogo husema ana hakika “amefunga” Kisauni. Bw Joho alikuwa mbunge wa eneo hilo kabla awe gavana.

Katika Kaunti ya Kilifiiliyo na jumla ya maeneobunge saba, KilifiKaskazini lililo na wapigakura 117,893, Malindi (95,593) na KilifiKusini (96,897) yanatarajiwa kuvutia ushindani mkubwa wa kura za kaunti.

Baadhi ya wanaotaka kurithi kiti cha Gavana Amason Kingi ni Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, na waziri msaidizi wa ugatuzi anayeondoka,

Bw Gideon Mung’aro, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa KilifiKaskazini. Awali Bw Mung’aro alikuwa mbunge wa Malindi kabla igawanywe mara mbili mwaka wa 2012.

Kaunti ya Kwale iliyo na maeneobunge manne inatarajiwa kuvutia ushindani mkubwa katika maeneo ya Kinango ambapo wapigakura waliosajiliwa ni 96,056, Matuga (80,553) na Msambweni (79,777).

Kwingineko katika Kaunti ya Taita Taveta, wagombeaji viti vya kuwakilisha kaunti wanatarajiwa kutilia maanani kura za Voi (59,725), Mwatate (45,214) na Taveta (40,250).

Mbunge wa Mwatate, Bw Andrew Mwadime, ni mmoja wa wanasiasa ambao wameonyesha nia ya kupigania ugavana kaunti hiyo dhidi ya Gavana Granton Samboja.

Kaunti ya Tana River iliyo na maeneobunge matatu, ina idadi kubwa ya wapigakura katika eneobunge la Garsen (53,669) huku Kaunti ya Lamu iliyo na maeneobunge mawili ikiwa na idadi kubwa Lamu Magharibi (59,055).

Vyama mbalimbali vya kisiasa vinajikakamua kutafuta ushindi hasa wa ugavana katika kaunti zote sita.

Katika uchaguzi ujao, ushindani unatarajiwa kuwa mkali zaidi kati ya mrengo wa Azimio la Umoja unaoongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga, na ule wa Kenya Kwanza unaomshirikisha Naibu Rais William Ruto wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Katika uchaguzi uliopita, ODM ilishinda ugavana katika Kaunti za Mombasa, Kilifina Tana River huku Jubilee ikishinda katika kaunti za Lamu na Kwale. Chama cha Wiper kilifanikiwa kushinda kiti cha ugavana katika kaunti ya Taita Taveta.

Kufikia sasa, magavana wa kaunti zote za Pwani wanaegemea Azimio la Umoja isipokuwa Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya ambaye anaegemea UDA.

  • Tags

You can share this post!

Nesi anayeuguza wagonjwa kwa nyimbo atuzwa

Pelicojam yapania kushiriki kipute cha Afrika mashariki na...

T L