• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Maoni yaweka Raila hatua kadhaa mbele ya Ruto

Maoni yaweka Raila hatua kadhaa mbele ya Ruto

WANDERI KAMAU NA MARY WANGARI

MWANIAJI urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga, anaongoza kwa umaarufu uchaguzi mkuu wa Agosti unapoendelea kukaribia kulingana na kura ya maoni ya Infotrak.

Kulingana na maoni hayo, Bw Odinga na mgombea-mwenza wake Martha Karua, wanaongoza kwa asilimia 42 huku Naibu Rais William Ruto na mwenza wake Rigathi Gachagua wakiwa na asilimia 38.

Ripoti hiyo inasema uchaguzi mkuu ungefanyika leo Bw Odinga angezoa jumla ya kura 9.3 milioni huku Dkt Ruto akipata 8.4 milioni.

Ripoti hiyo pia ilieleza kuwa Bw Odinga anaongoza katika kaunti 20, huku Dkt Ruto akiongoza katika kaunti 16.

Wawaniaji wengine wa urais wangepata asilimia moja ya kura, huku asilimia 19 ya Wakenya wakiwa bado hawajaamua kuhusu mwaniaji urais watakayemchagua.

Kando na Bw Odinga na Dkt Ruto, wawaniaji wengine wa urais ni Mwaure Waihiga (Agano Party of Kenya) na Profesa George Wajackoyah wa Roots Party of Kenya.

Wanne hao waliidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumatatu kuwania urais.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Infotrak, Angela Ambitho alisema utafiti huo ulifanyika kati ya Mei 27 na 29 katika kaunti zote 47.

Bw Odinga anaongoza katika maeneo ya Pwani (asilimia 49), Kaskazini (asilimia 49), Mashariki (asilimia 41), Nyanza (asilimia 73), Magharibi (asilimia 48) na Nairobi (asilimia 50).

Naye Dkt Ruto anaongoza katika maeneo ya Mlima Kenya (asilimia 52), Kusini mwa Bonde la Ufa (asilimia 59) na Kaskazini mwa Bonde la Ufa (asilimia 56).

Bi Ambitho alisema kaunti 11 katika maeneo ya Pwani, Bonde la Ufa, Kaskazini na Magharibi ndizo zitaamua yule atakayeibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Kaunti hizo ni Tana River, Kwale, Lamu, Turkana, Narok, Kajiado, Samburu, Nakuru, Pokot Magharibi, Bungoma na Trans Nzoia.

Alisema utafiti huo ulifanywa baada ya wawaniaji kuwateua wagombea-wenza wao.

Kwenye utafiti uliotolewa Mei 27, Dkt Ruto na Bw Odinga walikuwa na umaarufu sawa wa asilimia 42.

“Matokeo haya yanaonyesha athari za kisiasa za vigogo hao wawili baada yao kuwateua wagombea-wenza wao,” akasema Bi Ambitho.

Baadhi ya masuala makuu yanayoonekana kuwakera Wakenya wengi ni gharama ya juu ya maisha, uchukuzi na hali duni ya miundomsingi, ukosefu wa ajira, kupata maji safi, afya, elimu bora, gharama ya kufanya biashara kati ya mengine.

Kwenye kampeni zao, Bw Odinga na Dkt Ruto wamekuwa wakitoa ahadi za kuweka mikakati kufufua uchumi wa nchi ikiwa watachaguliwa kuwa rais.

  • Tags

You can share this post!

Shirika la Reli kuongeza safari za treni Kisumu

Ruto amponda Raila kuhusu mitumba

T L