• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Meza wembe, Kibicho amwambia Ruto

Meza wembe, Kibicho amwambia Ruto

GEORGE MUNENE NA BENSON MATHEKA

KATIBU wa Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, amepuuza wito wa Naibu Rais William Ruto na washirika wake wanaomtaka ajiuzulu kwa kujiingiza katika siasa.

Akijibu Naibu Rais na washirika wake, Dkt Kihicho aliwataka wameze wembe au wajinyonge kwa kuwa hatabanduka.

Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakimtaka Dkt Kibicho na baadhi ya mawaziri wajiuzulu au wafutwe kazi kwa sababu ya kujihusisha na siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza Ijumaa katika Shule ya Sekondari ya St Philips Baricho, Kaunti ya Kirinyaga, Dkt Kibicho alijitetea akisema kuwa anawahamasisha Wakenya kuhusumasuala ya siasa yanayoendelea nchini ili kuwasaidia kufanya maamuzi bora ifika – po uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

“Nitaendelea kujihusisha na masuala ya kisiasa. Wakipenda wameze wembe au wajitie kitanzi,” akasema Dkt Kibicho.

Waziri huyo alisema ataendelea kutoa maoni yake kuhusiana na siasa za humu nchini akisisitiza kuwa ana haki ya kufanya hivyo kama raia wengine.

“Nina haki yangu kumwelezea mama yangu namna ya kupiga kura ili aweze kumchagua kiongozi anayefaa. Ni jukumu langu kumwongoza kuhusiana na masuala ya kisiasa,” alisema Dkt Kibicho.

Wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais wamekuwa wakiwataka mawaziri na maafisa wakuu wa serikali hasa Dkt Kibic – ho, Waziri wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na Waziri wa Teknolojia ya habari na Mawasiliano, Joe Mucheru kujiuzulu akidai wanampendelea mpinzani wake mkuu, kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Kwa upande wake, Dkt Kibicho aliamrisha wanaochochea vurugu kwenye hafla za kisiasa wakamatwe mara moja.

Wiki jana alisema atatekeleza majukumu yake ipasavyo na kwamba hatasita kuwanyoosha wanaochochea ghasia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Alionya pia kuwa atakayechochea vurugu atachukuliwa hatua. Mnamo Novemba 1 alipendekeza wanaoenda kinyume na ajenda za Rais Kenyatta waadhibiwe.

“Sasa hivi nchi iko katika hatua za kampeni. Yeyote atakayepatikana akichochea vurugu ataadhibiwa vikali. Tuna vitoa machozi na silaha nyingi kwenye ofisi zetu. Tutazitumia vilivyo,” akaonya Dkt Kibicho.

Alieleza kuwa serikali iko macho na haitamhurumia yeyote atakayeleta fujo wakati huu wa kampeni.

Washirika wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu Dkt Kibicho kwa misimamo yake mikali ya kutetea serikali ya Rais Kenyatta.

Kulinganana mbunge wa Soy, Caleb Kositany, ni Wakenya wanaotumia mamlaka yao kuhangaisha wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa serikali.

“Kibicho amezidi, watu watakunyorosha kabla ya kuwanyorosha,” Bw Kositany alisema kwenye Twitter, katibu huyo alipopendekeza wanaokaidi Rais Kenyatta waadhibiwe. Mawaziri Matiang’i, Peter Munya( kilimo), Eugene Wamalwa( ugatuzi) na Joe Mucheru pia wamepuuza wito wa Dkt Ruto na washirika wake waache siasa.

Bw Matiang’i amewashauri maafisa wa serikali kutotishwa na wanasiasa wanapotekeleza majukumu yao. “Msitishwe.

Mnawajibika kwa raia wa Kenya na kazi yenu ni kutowavumilia wanaohusika na ghasia za uchaguzi,” Bw Matiang’i amekuwa akisema na kuongeza kuwa anapokea na kufuata maagizo kutoka kwa Rais Kenyatta pekee.

You can share this post!

Hofu kuu ya Ruto ni kuibiwa kura 2022

Kinaya Ruto akiita mawaziri wanaomkosoa

T L