• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Moi amtaka Ruto kukomesha siasa za 2022

Moi amtaka Ruto kukomesha siasa za 2022

Na FLORAH KOECH

SENETA wa Baringo Gideon Moi amepuuzilia mbali azma ya urais ya Naibu Rais William Ruto hapo 2022, akimtaka kutumia nguvu zake kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuwaambia waamini ndoto yake ya kuwa kiongozi wa nchi.

Seneta huyo amepuuzilia mbali mijadala yote ya siasa za 2022 na kuwataka viongozi kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza ajenda za maendeleo kwa wananchi.

Bw Moi amesema kwamba ni mapema mno kwa Wakenya kuanza kulazimishiwa siasa za 2022 wakati ambapo taifa hili linakabiliwa na changamoto nyingi.

“Kwa sasa tuangazie masaibu yanayowakumba wananchi na tukomeshe siasa hadi pale wakati wake utafika. Tunapaswa kuzungumzia kuhusu miradi ya maendeleo, si kukita kwa siasa,” akasema kiongozi huyo wa chama cha KANU mjini Kabarnet.

Vita vya udhibiti wa kura za eneo la Bonde la Ufa vinaonekana kuanza na Kaunti ya Baringo ndiyo uwanja wa malumbano ya kisiasa baina ya Naibu Rais William Ruto na seneta huyo.

Wakati huo huo, alisifu mdahalo unaoendelea kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga, akisema hatua hiyo ni kwa ajili ya umoja wa kitaifa na wala si siasa hewa.

“Kusalimiana kwa mkono kati ya Rais na Bw Odinga kumeiletea nchi hii umoja ambao unahitajika na kila mwananchi,” akasema.

Pia, aliitaka serikali ya kitaifa kuharakisha mpango wa kuzitumia serikali za kaunti pesa, akitaja kuwa kucheleweshwa kwake kumelemaza maendeleo mashinani.

Seneta huyo aliitaka serikali iwafidie waathiriwa wote wa wizi wa mifugo na kuwapa ardhi ya kuishi watu wote waliohama makwao North Rift.
Alisema kwamba watu waliolazimika kuhama makwao tangu 2005 kutokana na uvamizi wanafaa kusajiliwa kama wahamiaji wa ndani.

Bw Moi aliashiria kutoridhishwa na serikali kusalia kimya wakazi wakizidi kutoroshwa makwao.

“Tutaishukuru serikali wakati itaelewa masaibu wanayopitia watu wa jamii za eneo hili kutokana na uvamizi wa wezi wa mifugo. Tunahitaji hatua za kukomesha hali hii,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa viongozi kutoka jamii zinazopigania mifugo wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuletea eneo hilo amani.

“Kulaumiana hakutaleta suluhu yoyote. Tunafaa kuongoza juhudi za kupata suluhu kwa kuwaunganisha watu wetu na kusameheana iwapo tunalenga kuona maendeleo halisi,” akasema.

 

 

You can share this post!

Kamworor na Jepkosgei wasema wanalenga juu zaidi 2018

Muungano mpya wanukia Mudavadi akinyemelea Ruto

adminleo