• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Mswada wa mbunge kuinua sekta ya sukari

Mswada wa mbunge kuinua sekta ya sukari

Na BRIAN OJAMAA

MBUNGE wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi amesema kuwa mswada kuhusu sekta ya sukari aliowasilisha Bungeni unalenga kuboresha maisha ya wakulima wa miwa.

Bw Wamunyinyi aliyekuwa akihutubia wakazi wa eneobunge hilo Jumamosi, alisema mswada huo utaanza kujadiliwa Bunge la Kitaifa litakaporejelea shughuli zake mnamo Juni 8, mwaka huu.

“Nimebuni mswada ambao utajadiliwa bunge litakaporejelea shughuli zake mwezi ujao,” akasema.

Mbunge huyo alisema kuwa mswada huo unapendekeza kurejeshwa kwa bodi za miwa ambazo zitakuwa na wawakilishi wa wakulima. Alisema mswada huo unalenga kutatua changamoto zote zinazokabili sekta ya sukari nchini.

“Wakulima wanahangaika kwa miezi mingi kukuza miwa na kisha kuvuna na kuipeleka viwandani. Lakini wakulima hawalipwi na wafanyakazi wa viwandani pia hawapewi mishahara ilhali wasimamizi wanapora mamilioni ya fedha,” akasema Bw Wamunyinyi.

Alisema wakulima wengi wa miwa hawawezi kulipia watoto wao karo ya shule kutokana na umaskini. “Kwa mfano, kiwanda chetu cha sukari cha Nzoia kinakaribia kusambaratika,” akasema.

Mwezi uliopita, Bw Wamunyinyi alifanya kikao cha dharura kati ya viongozi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia na wakulima wa miwa – hatua iliyonusuru Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Nzoia Michael Makokha dhidi ya ghadhabu za wakulima.

Wakulima wa miwa, wafanyakazi wa kiwanda hicho na wanaharakati wa kutetea haki walikuwa wakiandamana wakitaka Bw Makokha ang’atuke kwa madai ya usimamizi mbovu wa kiwanda.

Wamunyinyi ambaye ni mbunge wa eneo hilo, aliitisha mkutano wa dharura katika Wadi ya Bukembe Mashariki ili kupatanisha pande husika.

Wakulima walipanga kumtimua Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye walidai ameshindwa kuwalipa deni lao la Sh465 milioni. Wakulima walisema kwamba hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miezi saba.

Lakini Bw Makokha alimtaka mbunge huyo na Kamishna wa Kaunti ya Bungoma Samuel Kimiti kutuliza wakulima kwenye kikao kilichodumu kwa muda wa saa tano.

Bw Wamunyinyi alisema kuwa wakulima hao walikubali kufutilia mbali maandamano na kumpa Mkurugenzi Mtendaji makataa ya mwezi mmoja kutekeleza mambo yaliyoafikiwa kwenye kikao hicho.

Miongoni mwa masuala walioafikiana ni kuwalipa wakulima fedha zao ndani ya mwezi mmoja baada ya kuwasilisha miwa yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho pia aliahidi kuhakikisha kuwa wakulima wa miwa wanalipwa malimbikizi madeni na wafanyakazi kupewa mishahara yao.

You can share this post!

Wakazi Vihiga wakusanya saini kuvunja serikali ya kaunti

Maelfu watoroka makwao baada ya volkano kulipuka