• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Mudavadi kuwa tu waziri katika serikali ya Ruto

Mudavadi kuwa tu waziri katika serikali ya Ruto

NA ONYANGO K’ONYANGO

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, amepoteza nafasi ya kuwa mwaniaji mwenza wa Naibu Rais Wiliam Ruto, baada ya muungano wa Kenya Kwanza kukosa kusajiliwa kuwa chama.

Leo Jumamosi ndiyo siku ya mwisho ya kusajili miungano kuwa chama katika afisi za Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Kenya Kwanza inashirikisha vyama vya UDA, ANC na Ford Kenya.

Kwa kuwa Dkt Ruto atakuwa akiwania urais kupitia chama cha UDA, mgombea mwenza wake pia lazima atoke chama hicho kulingana na sheria.

Kwa mujibu wa sheria mpya, makubaliano ya miungano lazima yawasilishwe katika afisi ya Anne Nderitu kufikia Aprili 9 (leo), miezi minne kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mnamo Januari, Rais Uhuru Kenyatta alitia saini Mswada wa Vyama vya Kisiasa ambao uliruhusu miungano isajiliwe kama vyama vya kisiasa.

Hadi sasa ni muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, anaolenga kutumia Kinara wa ODM Raila Odinga, ndio pekee umesajiliwa kama chama cha kisiasa.

Hapo jana Ijumaa, Bi Nderitu alithibitishia Taifa Leo kuwa ni muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya pekee ambao umesajiliwa kama chama katika afisi zake.

“Ni Azimio pekee ambayo imewasilisha makubaliano ya muungano wao. Aprili 9 ndiyo siku ya mwisho kwa miungano ya kisiasa kusajiliwa, ila makataa ya muungano wa kawaida bado ni Mei 8,” akaeleza Bi Nderitu.

Mwenyekiti wa UDA, Bw Johnstone Muthama, alisema Ijumaa kuwa hawajakubaliana iwapo Kenya Kwanza ingesajiliwa kama chama, na kwamba mazungumzo yalikuwa yakiendelea.

“Hatujasajili Kenya Kwanza ila jina hilo limehifadhiwa. Siwezi kufichua iwapo itakuwa muungano ambao utasajiliwa kama chama kwa sababu mashauriano bado yanaendelea. Yote yatafahamika baada ya makataa ya Aprili 9,” akasema Bw Muthama.

Jina la KKA lilihifadhiwa na Bw Mudavadi kupitia mkuu wa wafanyakazi katika afisi yake, Bw Godfrey Kanoti, mwaka 2021.

Wakati huo MaBw Mudavadi na Wetang’ula bado walikuwa katika muungano wa OKA.

Usajili huo ulitokana na vinara wa OKA kutoaminiana kwani muungano wenyewe ulikuwa umesajiliwa na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali na mwenzake wa Kimilili Didmus Barasa, jana Ijumaa walisisitiza kuwa Naibu Rais atawania urais kupitia UDA wala si Kenya Kwanza.

“Atatumia UDA ndio maana amekuwa akiuza chama hicho kivyake licha ya kuwa ndani ya Kenya Kwanza. Kwa sasa ni UDA inafaa kumtoa mwaniaji wa urais wala si muungano wa Kenya Kwanza,” akaeleza Bw Kang’ata.

Naye Bw Barasa alifafanua: “Kenya Kwanza ni muungano tu ambao vyama tanzu vilitia saini. William Ruto atawania urais kwa tiketi ya UDA wala si Kenya Kwanza.”

Aliongeza kuwa akina Mudavadi na Wetang’ula walielezwa vyema kuwa mgombeaji mwenza angetoka Mt Kenya walipoamua kushirikiana na Dkt Ruto.

Mbunge mmoja mwandani wa Dkt Ruto ambaye hakutaka jina lake linukuliwe alisema kuwa Mabw Mudavadi, Wetang’ula hawangeweza kupata wadhifa wa mgombeaji mwenza kwa sababu walianza tu ushirikiano na Naibu Rais mwaka huu 2022.

Hata hivyo, Katibu wa ANC Simon Gikuru aliwashutumu wenzake wa UDA akishikilia kuwa Kenya Kwanza imetimiza vigezo vyote vinavyohitajika na Msajili wa vyama vya kisiasa kabla ya makataa ya leo Jumamosi.

  • Tags

You can share this post!

PSG kumpa Mbappe ofa mpya ya Sh23.4 bilioni ili asihamie...

TUSIJE TUKASAHAU: Tungali tuna kibarua kutokomeza ukeketaji

T L