• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:26 PM
PSG kumpa Mbappe ofa mpya ya Sh23.4 bilioni ili asihamie Real Madrid msimu huu

PSG kumpa Mbappe ofa mpya ya Sh23.4 bilioni ili asihamie Real Madrid msimu huu

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamefichua mpango wa kumpokeza mshambuliaji Kylian Mbappe ofa mpya ya Sh23.4 bilioni ili atie saini mkataba mpya wa miaka miwili zaidi kambini mwa kikosi hicho.

Kandarasi ya sasa kati ya PSG na Mbappe, 23, inatamatika mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22 na inaaminika kwamba nyota huyo raia wa Ufaransa tayari aliafikiana na Real Madrid miezi michache iliyopita kuyoyomea ugani Santiago Bernabeu kwa Sh21 bilioni kufikia Julai 2022.

Kwa mujibu wa mkataba mpya ambao PSG wanajiandaa kumpa Mbappe, sogora huyo wa zamani wa AS Monaco ya Ufaransa atakuwa akitia mfukoni mshahara wa Sh3.3 bilioni kwa mwaka.

Licha ya ofa hiyo nono, inaarifiwa kwamba matamanio ya Mbappe ni kuondoka PSG na kuingia katika sajili rasmi ya Real.

Akihojiwa na wanahabari baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyokutanisha PSG na Lorient mnamo Aprili 3, 2021, Mbappe alisema: “Bado sijafanya maamuzi kuhusu mustakabali wangu kitaaluma. Kuna vigezo kadhaa ambavyo nitazingatia kisha nishauriane na wadau kadhaa kabla ya nijiamulie iwapo ni kusalia PSG au kuelekea kwingineko.”

Mawakala wa Mbappe ni wazazi wake ambao pia wametofautiana kuhusu iwapo huu ni wakati mwafaka kwa mwanao kuondoka PSG au la. Iwapo sogora huyo atahiari kusalia PSG basi washauri wake wakuu watapokea kiinua mgongo cha Sh6.6 bilioni kutoka kwa mabwanyenye wa Qatar wanaomiliki kikosi hicho.

Iwapo ofa mpya ya PSG itamshawishi Mbappe kusalia ugani Parc des Princes, Real wamefichua kwamba watawania huduma za mshambuliaji chipukizi wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Norway, Erling Braut Haaland ambaye pia anamezewa mate na Barcelona, Manchester City na Manchester United.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Maonevu dhidi ya timu za Kenya zikicheza ugenini...

Mudavadi kuwa tu waziri katika serikali ya Ruto

T L