• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Nassir adai Kalonzo ana nia fiche dhidi ya Odinga

Nassir adai Kalonzo ana nia fiche dhidi ya Odinga

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita Abdulswamad Nassir amedai kuwa kinara Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, alimshurutisha aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kutaka ugavana Mombasa, ili kuharibu kura za mgombea wa urais wa Azimio La Umoja Bw Raila Odinga.

Alimuonya Bw Musyoka dhidi ya kusambaratisha muungano wa Azimio La Umoja.

“Wacha kuingilia siasa za Mombasa kwa kumsukuma Bw Sonko Mombasa. Mwezi mmoja hivi uliopita nilisafiri na Bw Sonko na hakunieleza kuwa anapanga kutaka kiti hiki. Kama Kalonzo ana haja sana na Mombasa, si angelikuja mwenyewe? Mbona atumane,” akauliza Bw Nassir.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Bw Nassir alisema Bw Musyoka alifanya kusudi kumtuma Bw Sonko, ambaye aliondolewa mamlakani na Bunge la Kaunti ya Nairobi mnamo 2020, kulumbana na Bw Odinga.

“Anatuma wanasiasa kuwania viti katika sehemu ambazo Bw Odinga ana ufuasi mkubwa, ili kugawanya kura zake. Ni mchezo wa paka na panya tu lakini tushamgundua. Bw Sonko hana makosa yeye ni mtumwa tu,” alisema Bw Nassir.

Aliwonya wakazi wa Mombasa dhidi ya kumpigia kura mgombea wa UDA Bw Hassan Omar, na pia kukana madai kuwa alishurutishwa na Gavana Hassan Joho kuwa mrithi wake.

Bw Nassir alisema amekuwa mstari wa mbele kuikashifu serikali ya kaunti hasa katika masuala ya majitaka.

“Lazima watu wawajibike kama kuna mlipuko wa maradhi kwa sababu ya majitaka? Kuna watu wamenishutumu kwa kukosoa serikali ya kaunti. Nihukumu kwa makosa yangu,” alisisitiza Bw Nassir.

Kwa swala la changamoto ya maji, Bw Nassir alisema litatatuliwa endapo wawekezaji watahusishwa kusafisha maji ya baharini.Mombasa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji.

Alimshukuru Bw Suleiman Shahbal kwa kumuunga mkono. Alisema amekutana na Bw Shahbal mara kadhaa na wameamua kushirikiana.

“Ananisaidia sana kwenye azma yangu, ninawasihi wale waliokuwa mrengo wake kujiunga nami. Awali kulikuwa na mgogoro lakini tumesuluhisha kila kitu. Kura ya maoni ilitumiwa kumsaka atakayepeperusha bendera ya ugavana Mombasa. Lakini kwenye siasa uwaminifu ni muhimu sana,” Bw Nassir aliongeza.

Kwenye mahojiano na runinga moja, Bw Sonko alisema kwamba alikuwa akiwazia kugombea kiti chake cha Nairobi lakini akaambiwa na Bw Musyoka asithubutu.

“Bw Musyoka ndiye aliyeamua niwanie ugavana Mombasa. Aliniambia jijini Nairobi nitakabiliwa na vita vikali, na sababu ninamheshimu nikakubali. Sikukataliwa na wakazi wa Nairobi. Ni serikali ndio iliniondoa,” akasema gavana huyo wa zamani.

Juzi, Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alijitokeza kuweka mambo wazi kwamba hakutia saini ya makubaliano yoyote ya kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu Agosti 9.

Hata hivyo alisema yuko tayari kutetea kiti cha ubunge Kisauni endapo ataidhinishwa na wapiga kura wake.

Mbunge huyo wa Kisauni alipewa asilimia 60 ya uongozi wa kaunti katika makubaliano uliosimamiwa na Kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka ambapo Bw Sonko alipewa tikiti ya kuwania ugavana wa Mombasa.Wengine wanaowania ugavana ni naibu gavana Dkt William Kingi (Pamoja African Alliance), aliyekuwa seneta wa Mombasa Bw Hassan Omar (United Democratic Alliance) na aliyekuwa mbunge wa Nyali Bw Hezron Awiti (VDP).

Bw Sonko naye alisema Bw Mbogo alikuwa hataki kuwa mgombea wake mwenza lakini alishawishiwa na Bw Musyoka.

Bw Sonko alijitetea katika kujitosa katika kinyanganyiro hicho cha Mombasa akisema yeye ni mzaliwa wa pwani.

“Wale wasionielewa, mimi ni mzaliwa wa Pwani, mamangu alizikwa humo humo kwa hivyo naelewa eneo hilo zaidi kuliko kila mtu. Wale wanasema Sonko ametoka bara kuja kuchukua kiti Mombasa wanapotosha Wakenya. Mtu yeyote anaweza kugombea kiti cha siasa kokote nchini,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Beki Ronald Araujo sasa kuchezea Barcelona hadi 2026

Aliyenajisi watoto sasa atabaki jela kwa miaka 46

T L