• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
OKA, Raila wataungana kukabili Ruto 2022 – Lenku

OKA, Raila wataungana kukabili Ruto 2022 – Lenku

Na STANLEY NGOTHO

GAVANA Joseph Ole Lenku wa Kajiado amedai kwamba ana “ujasusi” kwamba kiongozi wa ODM, Raila Odinga, na muungano wa Okoa Kenya Alliance (OKA) watabuni serikali ijayo.

Hivyo, aliirai jamii ya Wamaasai kuunga mkono mrengo wa handisheki, akisema ndio utaibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.Akiwahutubia wafuasi wake wikendi katika eneo la Kajiado ya Kati, Bw Lenku alisema anajua siri fiche ya serikali kuhusu uchaguzi huo.

Alisema hayo kwenye hafla ya shukrani ya Naibu Gavana Martin Motisho.Bw Lenku alisema Bw Odinga ataungana na vinara wa muungano wa OKA kubuni muungano mkubwa wa kisiasa ili kumkabili Naibu Rais William Ruto kwenye kinyang’anyiro cha urais.

“Nilikuwa Waziri wa Usalama wa Ndani katika serikali ya Jubilee. Hivyo, ninafahamu jinsi serikali huwa inaendesha mipango yake. Bw Odinga ataungana na viongozi wa OKA hivi karibuni na watabuni serikali ijayo chini ya mpango wa ‘Azimio la Umoja’,” akasema Bw Lenku.

Aliirai jamii hiyo kuunga mkono mpango huo, ili kutojipata nje ya serikali baada ya uchaguzi ujao.Alionekana kuwalenga baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakimuunga mkono Dkt Ruto kwenye kampeni zake katika sehemu mbalimbali nchini.

Bw Lenku alisema kuwa jamii za kuhamahama zitakuwa salama chini ya serikali ya Bw Odinga badala ya Dkt Ruto.

You can share this post!

Polisi chonjo kukabili magenge msimu huu

Biden, Putin kujadiliana taharuki ya Marekani, urusi kuhusu...

T L