• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Oparanya akaripia Mudavadi, Weta’ kuhusu maendeleo

Oparanya akaripia Mudavadi, Weta’ kuhusu maendeleo

NA BENSON AMADALA

GAVANA wa Kakamega, Wycliffe Oparanya, amemtaka kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula kuelezea miradi waliyoanzisha walipokuwa wakishikilia nyadhifa kubwa kubwa serikalini.

Bw Oparanya aliwataka Mabw Mudavadi na Wetang’ula kukoma ‘kuhadaa’ wakazi wa Magharibi kwa kuwapa ahadi tele wanazodai zitatimizwa na serikali ya Kenya Kwanza iwapo mwaniaji wake wa urais William Ruto atashinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Gavana Oparanya ambaye anaongoza kampeni za Azimio la Umoja One Kenya katika eneo la Magharibi, alisema ahadi zinazotolewa na wanasiasa wa Kenya Kwanza hazina mashiko.Alisema Mabw Mudavadi na Wetang’ula wamewahi kushikilia nyadhifa za juu katika serikali za Rais Daniel Moi na Mwai Kibaki ‘lakini hakuna miradi waliyoanzisha eneo la Magharibi’.

Bw Oparanya alisema ilikuwa aibu kwa Bw Mudavadi kumsihi Rais Kenyatta kutia lami katika barabara inayoelekea nyumbani kwake kijijini Sabatia wakati wa mazishi ya mama yake ilhali amewahi kuhudumu kama makamu wa rais na Waziri wa Fedha.

“Nimeshangaa kwamba viongozi kama vile Mudavadi, Wetang’ula, Benjamin Washiali na Ababu Namwamba wamekuwa wakishambulia kiongozi wa Azimio Raila Odinga. Wamekuwa wakidai kuwa Bw Odinga hajafanyia jamii ya Waluhya chochote ilhali wao pia wamewahi kushikilia nyadhifa za juu serikalini na walishughulikia masilahi yao ya kibinafsi na kusahau watu wa Magharibi,” akasema.

Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula katika kampeni zao eneo la Magharibi wamekuwa wakishutumu Bw Odinga kwa kutumia jamii ya Waluhya kupata kura tu na kisha kuwatelekeza.

“Tumechoka kujaribu kumsukuma kuwa rais kila baada ya miaka mitano. Amekuwa mzigo kwetu na hatutaendelea kumuunga mkono,” alisema Bw Wetang’ula alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Bomani mnamo Juni 17.

Viongozi wa Kenya Kwanza wameahidi kuimarisha kampeni zao katika eneo la Magharibi ili kuhakikisha Dkt Ruto anapata asilimia 90 ya kura.

“Tunataka kumfungia Raila nje ya eneo la Magharibi. Ametutumia vibaya kwa muda mrefu,” alidai Bw Wetang’ula.

Lakini Gavana Oparanya alisema kuwa Mabw Mudavadi na Wetang’ula hawana mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya jamii ya Waluhya.

“Wawili hao wanafaa kukoma kutumia jina la Waluhya kujinufaisha wao binafsi. Wawili hao wanatumiwa na Dkt Ruto kujaribu kupata kura katika eneo la Magharibi.

“Tunajua kuwa Bw Mudavadi alipewa hela ili kuzima azma yake ya kuwania urais. Yeye ni kama Esau katika Biblia ambaye aliuza baraka zake kwa sahani ya chakula,” akadai.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Polisi wasiegemee mrengo wowote...

DARUBINI YA UKWELI: Ripoti ya TJRC inarejelea Vita vya...

T L