• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Raila: Chebukati anafaa kuwa jela

Raila: Chebukati anafaa kuwa jela

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa Azimio la Umoja, Raila Odinga anataka Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, Wafula Chebukati achukuliwe hatua kali kisheria akirejelea msimamo wake wa kutangaza matokeo tata ya uchaguzi wa urais uliofanyika mnamo Agosti 9, 2022.

Amedai kwamba hatua ya Bw Chebukati ilinyima Wakenya fursa ya kuchagua kidemokrasia rais wanayemtaka.

Akimtaja Bw Chebukati kama ‘mhalifu’, Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema anapaswa kuwa akihudumu kifungo cha jela.

Bw Odinga alisema hatua ya mwenyekiti huyo wa tume kutangaza matokeo yaliyokataliwa na baadhi ya makamishna, ni uhalifu wa kiuchaguzi ambao kulingana naye anafaa kuadhibiwa kisheria.

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne usiku, kiongozi huyo wa ODM alisema Chebukati anapaswa kufunguliwa mashtaka na kuhukumiwa.

“Chebukati ni mhalifu anayepaswa kushtakiwa na kuwekwa jela,” akasema.

Uchaguzi mkuu uliopita, Odinga alipinga matokeo ya kura za urais katika mahakama ya upeo jopo lililoongozwa na Jaji Mkuu, Bi Martha Koome likifutilia mbali malalamishi yake na kuidhinisha ushindi wa Rais William Ruto (Kenya Kwanza).

Hata ingawa aliitikia maamuzi ya mahakama, anasema korti ilichukulia ‘kiholela’ kesi aliyowasilisha akitaja lugha iliyotumiwa na majaji wakati wakiainisha vigezo alivyoibua kama yenye kiburi.

Kabla Chebukati kutoa rasmi matokeo, IEBC ilishuhudia mgawanyiko makamishna wanne ndio naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi wakijitenga na kuyakataa.

Odinga aidha alitaja hatua hiyo kama ya kihistoria nchini, tume kugawanyika.

Akionekana kuendeleza mashambulizi yake kwa mwenyekiti wa tume, alidai “Chebukati ndiye alichangia mgawanyiko na mambo kuharibika katika kituo kikuu cha kujumlisha kura katika ukumbi wa Bomas of Kenya”.

“Ni kwa bahati mbaya alichochea mgawanyiko, akatangaza matokeo ambayo yeye mwenyewe anajua alikotoa,” akaelezea.

Dkt Ruto ameunda kamati inayoongozwa na Jaji Aggrey Muchelule kuchunguza makamishna hao nne.

Watatu kati yao; Cherera, Nyang’aya na Wanderi hata hivyo walijiuzulu kabla vikao kuwahoji kuanza.

Odinga amekashifu kubuniwa kwa kamati hiyo, akiitaja kama haramu na inayokiuka kisheria.

Aidha, Raila anataka ukaguzi wa matokeo kufanyika kuanzia vituo vya kupigia kura, maeneobunge hadi kituo kikuu cha kujumlisha akisema hatua hiyo itadhihirisha ukweli wa malalamishi yake.

  • Tags

You can share this post!

Onyo kwa wanaotishia wakazi Pwani

TANZIA: Vigogo wa soka watuma salamu za pole kufuatia kifo...

T L