• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:01 PM
Raila, Ruto kutumia mbinu mpya kuwinda kura kuanzia kesho Jumatatu

Raila, Ruto kutumia mbinu mpya kuwinda kura kuanzia kesho Jumatatu

NA LEONARD ONYANGO

WASHINDANI wakuu wa urais; kinara wa Azimio Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto wanatarajiwa kuanza kampeni motomoto kote nchini kuanzia kesho Jumatatu baada ya kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Odinga amepeleka stakabadhi zake kwa IEBC leo Jumapili katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, saa 4.00 asubuhi. Dkt Ruto aliidhinishwa Jumamosi kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto tayari amegawanya kikosi chake katika makundi matatu yatakayomsaidia kuwinda kura katika maeneo mbalimbali ya nchi. Vikosi hivyo vitaongozwa na Dkt Ruto, mwaniaji mwenza wake Rigathi Gachagua na kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudvadi.

Kikosi cha Naibu wa Rais kitajumuisha Magavana Amason Kingi (Kilifi), Moses Lenolkulal (Samburu) na Alfred Mutua (Machakos), wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini)), Kimani Ichung’wah (Kikuyu), M Peris Tobiko (Kajiado Mashariki) na Charles Kanyi, almaarufu Jaguar (Starehe).

Kikosi cha Mudavadi kitajumuisha magavana Okoth Obado (Migori), Samwel Tunai (Narok) na gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo, maseneta Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Catherine Waruguru (Laikipia).

Bw Gachagua ataongoza Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, waziri wa zamani Charles Keter, mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na mbunge wa kaunti ya Narok Soipan Tuya.

Kikosi cha Bw Gachagua kitakita kambi katika maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome za Naibu wa Rais kama vile Bonde la Ufa na Mlima Kenya.

Kikosi cha Bw Mudavadi kitaendesha kampeni katika maeneo ya Nyanza na Magharibi.

Dkt Ruto atatumia muda mwingi katika maeneo yanayochukuliwa kuwa uwanja wa mapambano kama vile Kajiado, Narok, Turkana, Pwani kati ya mengineyo.

Kikosi cha Dkt Ruto pia kitakuwa kikizuru mara kwa mara katika eneo la Mlima Kenya katika juhudi za kuzima ushawishi wa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga, Bi Martha Karua.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga ameunda vikosi 16 vitakavyomsaidia kuendesha kampeni katika maeneo yote ya nchi.

Hatua ya kinara wa Wiper kurejea katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, huenda ikasukuma Bw Odinga kuunda kikosi cha 17.

Kikosi cha kampeni cha eneo la Ukambani kwa sasa kinaongozwa na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na kinajumuisha mbunge wa Kitui Kusini Rachel Nyamai, mwaniaji wa ugavana wa Machakos Nzioka Waita na mwanasiasa Kibwezi Magharibi Seth Kakusye.

Bw Odinga hakujumuisha viongozi wa Wiper kwenye vikosi vyake vya kuwinda kura baada ya Bw Musyoka kugura Azimio mwezi uliopita akipinga kuteuliwa kwa Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza.

Afisa katika sekteriati ya kampeni za Bw Odinga aliambia Taifa Jumapili kuwa Bw Musyoka huenda akatwika jukumu la kusaka kura katika eneo la Mashariki linalojumuisha Ukambani na kaunti jirani kama vile Tharaka Nithi, Meru, Garissa kati ya mengineyo.

“Japo Bw Kalonzo ana ufuasi katika maeneo mbalimbali za nchi, ataelekeza nguvu zake katika eneo la Mashariki ili kuzima ushawishi wa Ruto.

“Musyoka pia atakuwa anaandamana na Bi Karua katika eneo la Mlima Kenya kusaka kura,” akasema.

Katika baadhi ya Kaunti, Bw Odinga amegawanya vikosi vya kuwinda kura katika makundi mawili; kikosi cha kampeni za urais na kikosi cha kupigia debe magavana wa Azimio.

Katika Kaunti ya Nairobi, mfanyabiashara Richard Ngatia anaongoza kampeni za Bw Odinga huku Gavana Anne Kananu akiongoza kampeni za mwaniaji wa ugavana wa Azimio Polycarp Igathe.

Bw Odinga anatarajiwa kesho kuorodhesha ahadi ambazo analenga kutekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa Agosti 9.

“Jumatatu nitaelezea Wakenya mambo nitakayofanya ndani ya siku 100 za utawala wangu baada ya kuwasilisha stakabadhi zangu kwa IEBC Jumapili (leo),” Bw Odinga aliambia wafanyabiashara wa Umoja wa Ulaya (EU) wiki iliyopita.

Naye, Naibu wa Rais Ruto anatarajiwa kuzindua manifesto yake Juni 30 baada ya vikosi vyake vitatu kuzunguka kote nchini.

  • Tags

You can share this post!

Kampeni kuchacha Boga, Mwakwere wakiidhinishwa kugombea

Mucheru adai Chebukati aibia Ruto siri

T L