• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mucheru adai Chebukati aibia Ruto siri

Mucheru adai Chebukati aibia Ruto siri

NA MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Joe Mucheru ameisuta Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa “kucheza karata” na sajili ya wapigakura kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Alisema kuna uwezekano kuwa tume hiyo imekuwa ikitoa maelezo kuhusu sajili hiyo kwa mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Alhamisi, katika mkutano na mabalozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Dkt Ruto alidai kuwa karibu wapigakura milioni moja kutoka ngome zake wamehamishwa kutoka vituo vyao hadi vingine, bila idhini yao.

Akiongea katika Kaunti ya Murang’a mnamo Ijumaa, Waziri Mucheru alisema hivi, “Malalamishi yangu ni kwamba IEBC inawaruhusu watu wengine kujua idadi ya watu walio katika sajili yake. Mwenyekiti alisema kuwa sajili hiyo itakuwa tayari kwa umma kujua yaliyomo lakini sasa tunasikia kuwa tayari watu wengine tayari wamepewa sajili hiyo ili kutoa kauli yao kuihusu.”

Bw Mucheru alisema hatua hiyo imesababisha watu fulani kudai kuwa wamegundua kuwa wapigakura wanahamishwa kutoka kituo kimoja hadi kingine.

“Hata sisi tunataka kupata nafasi ya kutazama sajili hiyo,” akasema.

Waziri Mucheru amekariri kila mara kwamba anaunga mkono mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga.

Hata hivyo, alijitetea dhidi ya shutuma alizoelekezewa na wafuasi wa Dkt Ruto kwamba analenga kuiba kura kumsaidia Bw Odinga kushinda katika kinyang’anyiro cha urais.

“Ikiwa hilo linaweza kufanyika ni IEBC ambayo inaweza kuhusika. Mimi kama mtu binafsi au sisi kama maafisa wa serikali hatushiriki katika uendeshaji wa uchaguzi,” akasema Bw Mucheru.

“Ni IEBC ndiyo huendesha masuala yanayohusiana na mitambo ya uchaguzi, sava na masuala yote kuhusu uchaguzi, sio sisi,” akaeleza.

Bw Mucheru alisema kuwa ni Mungu pekee ndiye atakayeamua viongozi watakaotwikwa wajibu wa kuendesha masuala ya nchi.

“Mungu ndiye atakayeongoza maamuzi yetu. Hatufai kuingiwa na wasiwasi kuhusu uamuzi huo,” akasema.

Ijumaa, Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, akihutubia mikutano ya kampeni jijini Nairobi, alimwonya Bw Mucheru dhidi ya kuiba kura za Dkt Ruto.

“Hebu ujitazame kwenye kioo na ujiulize ikiwa una uwezo wa kuiba kura za Dkt Ruto. Ukithubutu kufanya hivyo, utajua sisi ni akina nani,” Bw Nyoro akasema.

Hata hivyo, Ijumaa, Waziri Mucheru alisema kuwa wizara yake itaisaidia IEBC kuhakikisha inafanikisha shughuli ya utambuaji wa wapiga-kura, upigaji kura, ujumuishaji wa kura na upeperushaji wa matokeo.

“Kufikia sasa, kati ya vituo 53,000 vya kupigia kura, IEBC imetuambia kuwa 99 havijafikiwa na mtandao wa intaneti. Lakini jumla ya simu 1,500 zimenunuliwa kusuluhisha tatizo hilo kwa kusaidia katika upeperushaji wa matokeo,” akasema Bw Mucheru.

“Vile vile, tumeisaidia IEBC kupitia Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kwa kutoa leseni kwa kampuni za mawasiliano za Safaricom, Airtel na Telkom ambazo zitaweka mitandao kwa niaba ya IEBC,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Raila, Ruto kutumia mbinu mpya kuwinda kura kuanzia kesho...

Mwisho wa lami kwa Sonko kisiasa

T L