• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Ruto awanyooshea Uhuru na Raila mkono wa maridhiano

Ruto awanyooshea Uhuru na Raila mkono wa maridhiano

NA MARY WANGARI

RAIS Mteule William Ruto jana alisema wangali marafiki na Rais Uhuru Kenyatta licha yake kuchukua misimamo tofauti kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Akihutubia taifa saa chache baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wake, Naibu Rais alisema serikali yake itahakikisha kwamba Kiongozi wa Taifa anayeondoka anapatiwa heshima yake anapostaafu.

Huku akifichua kuwa hawajawasiliana na Rais Kenyatta kwa miezi kadhaa tangu watofautiane, Dkt Ruto alisema atampigia simu ili waafikiane kuhusu mchakato wa kupokezwa mamlaka.Alisema hana kinyongo wala kisasi dhidi ya Bw Kenyatta kufuatia uamuzi wake wa kumuunga mkono mpinzani wake mkuu, Raila Odinga.

“Nitampigia simu hivi punde rafiki yangu mzuri Rais Uhuru Kenyatta. Sijawasiliana naye kwa miezi kadhaa. Nitampigia ili tuzungumzie mchakato wa kubadilishana mamlaka,” alisema Dkt Ruto.

“Ninajua alijitahidi kwa njia yake binafsi, lakini Wakenya walifanya uamuzi wao. Sina chuki kabisa kwamba aliamua kumuunga mkono mgombea mwingine. Bado tungali marafiki. Nilipoamua kupigia debe azma ya urais ya Uhuru sikumpa masharti kwamba ni sharti angeniunga mkono. Sina kinyongo,” alisema.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa Rais Uhuru atapatiwa heshima yake anayostahili kama Kiongozi wa Taifa aliyestaafu.

“Tutampa heshima na hadhi yake anayostahili kama kiongozi wa taifa aliyestaafu. Sisi hatubebi visasi vya kipuzi. Amefanya kazi nzuri na jina lake litaandikwa katika historia ya Kenya,” alisema.

Rais Mteule vilevile aliwanyooshea mkono wa maridhiano wapinzani wake wakiongozwa na mshindani wake mkuu Bw Odinga, akiwahakikishia kwamba hakuna yeyote atakayelengwa na utawala wake.

Alisema kinyume na utawala uliopita, serikali yake haitatumia idara ya kukabiliana na uhalifu kuwanyanyasa watakaotofautiana naye kisiasa, akiwataka wapinzani wake wasiwe na hofu.

Alisema yuko tayari kuzika katika kaburi la sahau tofauti za kisiasa kati yake na Bw Odinga na kusisitiza kuwa serikali yake haina nafasi kwa handisheki.

“Raila Odinga atakapostaafu tutampa heshima anayostahili kama kiongozi wa kitaifa. Nitawasiliana vilevile na wapinzani wangu nikianza na Raila Odinga na timu ya Azimio ili tubuni jinsi ya kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya Wakenya. Kama nilivyosema, ninaamini katika sheria. Siamini hadithi za handisheki. Ninaamini katika serikali inayowajibika ikiangaziwa na upinzani unaowajibika,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru Kenyatta arudia makosa ya mlezi wake Moi katika siasa...

Montreal anayochezea Wanyama yang’ata Toronto MLS

T L