• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Ruto, Raila wapatana kuhusu masuala IEBC

Ruto, Raila wapatana kuhusu masuala IEBC

NA CHARLES WASONGA

USAHIHI wa sajili ya wapiga kura na utendakazi wa mitambo ya kielektroniki itakayotumika kuendesha uchaguzi na kupeperusha matokeo ni miongoni mwa masuala ambayo wagombea wawili wakuu wa urais wanataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wifafanue.

Mgombea urais wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA) William Ruto na mwenzake wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, wanasisitiza kuwa maelezo ya kuridhisha kuhusu masuala hayo ndio yatajenga imani ya umma kwamba uchaguzi mkuu ujao utaendeshwa kwa njia huru na ya haki.

Jana Jumapili, muda mfupi baada ya kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais, Bw Odinga aliitaka IEBC kutoa maelezo kuhusu hatua ambazo imepiga katika kusafisha sajili ya wapiga kura.

“Tunataka kujua ni lini sajili hiyo itakuwa tayari na kuwekwa wazi ili ikaguliwe na wadau wote na wapiga kura. Isitoshe, tunataka hakikisho kutoka kwa IEBC kwamba sajili sahihi itawekwa wazi kutoka ngazi ya wadi hadi kitaifa,” akasema.

Suala hili la hali ya usahihi wa sajili ya wapiga kura pia liliubuliwa na Dkt Ruto mnamo Alhamisi wiki jana alipofanya mkutano na mabalozi wa mataifa wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU).

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya United Democratic Alliance (UDA), alidai kuwa majina ya wapiga kura wapatao milioni moja kutoka ngome zake yameondolewa kutoka sajili ya wapiga kura ama yamehamishwa katika maeneo ya mbali. Dkt Ruto alidai hiyo ni njama ya kufanikisha wizi wa kura.

“Tunataka kila mhusika, ikiwemo EU kusaka maelezo kutoka kwa tume hii kuhusu jinsi karibu majina milioni moja yalitoweka kutoka sajili ya wapiga. Na mengi ya majina hayo ni ya watu kutoka maeneo ambayo ni ngome yetu. Ni wazi kwamba kuna hila fulani hapa,” Dkt Ruto akasema.

IEBC, kupitia mwenyekiti wake Wafula Chebukati, ilikubali kuwepo kwa dosari ambapo baadhi ya wapiga kura walijipata wamehamishwa kutoka vituo walikosajiliwa, lakini akasema kosa hilo linarekebishwa.

“Ni kweli tumepata ripoti kama hizo na tumechukua hatua ya kurekebisha kosa ambalo lilitokea. Ningependa kuwahikikisha Wakenya kwamba hatimaye sajili ya wapiga kura itakuwa sahihi kwa matumizi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9,” akasema Bw Chebukati.

MAJINA KUHAMISHWA

Baadhi ya wapiga kura kutoka eneo bunge la Nyeri Mjini waliohojiwa na kituo kimoja cha runinga wiki jana walidai kuwa majina yao yamehamishwa hadi Wajir.

Dkt Ruto na Bw Odinga pia wameitaka IEBC kutoa hakikisho kuhusu utendakazi wa mitambo ya kieletroniki ya kuwatambua wapiga kura na ile ya kupeperusha matokeo.

“Tunataka IEBC iitishe mkutano wa wadau wote ili kujadili suala la utendakazi wa mitambo yote ya kielektroniki itakayotumika katika uchaguzi mkuu ujao. Tunataka kujua ikiwa mitambo ya kuwatambua wapiga kura ni shwari sawa na ile ya kutuma matokeo kutoka vituo vya kupigia kura hadi vituo vya kujumuisha kura katika ngazi za kaunti na taifa,” Bw Odinga akasema Jumapili.

Suala hilo hilo liliibuliwa na mrengo wa Dkt Ruto katika barua iliyotumiwa IEBC na mkurugenzi wa jopo la kampeni zake za urais, Gavana Josphat Nanok wa Turkana.

“Tunataka IEBC ieleze hatua kwa hatua jinsi mitambo yake itafanya kazi, kuanzia kutambuliwa kwa wapiga kura hadi kupeperushwa kwa matokeo. Hii ni kutokana na mvutano uliopo sasa baada ya kufichuka kwamba baadhi ya vituo vya kupigia kura havijaunganishwa kwa mtandao wa 3G,” akasema Bw Nanok.

Jana Jumapili, Bw Chebukati alisema mitambo ya tume hiyo itafanyiwa majaribio mnamo Juni 9: “Tumewaalika wagombeaji wote wa urais siku hiyo ili washuhudie wenyewe utendakazi wa mitambo ambayo tutatumia Agosti 9.”

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, Jaji Mkuu Martha Koome pia aliitaka IEBC kuonyesha kwamba imeshughulikia masuala yote yaliyotumiwa na Mahakama ya Juu ilipofutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017.

“Mahakama ya Juu haikupata ushahidi wa mienendo mibaya ya wagombeaji bali ilipata kosa katika upeperushaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais. Kwa hivyo, IEBC inafaa kutoa hakikisho kwamba upeperushaji wa matokeo hautakumbwa na dosari tena,” Bi Koome alisema.

  • Tags

You can share this post!

Kiini cha mifugo kuvishwa ‘maski’

Uingereza yazama, Ujerumani ikila sare

T L