• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
SAMMY WAWERU: Nairobi inahitaji gavana atakayeiletea hadhi ya kimataifa

SAMMY WAWERU: Nairobi inahitaji gavana atakayeiletea hadhi ya kimataifa

Na SAMMY WAWERU

Maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Nairobi kumchagua gavana wa tatu yameshika kasi, baada ya vyama vikuu nchini kuidhinisha majina ya wanaomezea mate wadhifa huo na kuyawasilisha kwa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC).

Hatua hiyo itafungua awamu ya zoezi la mchujo vyamani, ili kuibuka na wagombea watakaopeperusha bendera kumrithi aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko aliyebanduliwa na madiwani na uamuzi huo kutiwa muhuri na bunge la seneti Desemba 2020.

Maseneta wapatao 27 walipiga kura kupitisha mswada wa MCA wa Nairobi kumuondoa Sonko mamlakani kwa madai ya kusakata ufisadi, ufujaji wa fedha za kaunti na matumizi mabaya ya ofisi.

Aidha, maseneta 16 walipiga kura kumnusuru huku 2 wakisalia ‘kimya’. Chama tawala cha Jubilee na kile cha upinzani ODM mnamo Jumatatu viliwasilisha majina ya wagombea kwa IEBC.

Aidha, Jubilee iliwasilisha majina ya aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini, Dennis Waweru na mfanyabiashara Agnes Kagure, ODM Sam Wakiaga na Beth Syengo.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu na ambaye alibanduliwa mapema 2020 kwa madai ya kushiriki ufisadi, ufujaji wa fedha, miongoni mwa kashfa zingine, aliwasilisha jina lake kwa IEBC kama mgombea wa kujitegemea.

Kaunti ya Nairobi ndiyo sura ya Kenya, kwa kuwa ndio mji mkuu. Wageni na watalii kutoka mataifa ya ughaibuni hutua nchini kupitia uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), hii ikiwa na maana kuwa wanalakiwa na jiji la Nairobi.

Ni mji unaopaswa kuwa na hadhi ya juu, kiwango cha usafi kikitakiwa kuwa cha kipekee.

Hata ingawa Idara ya Ustawishaji Jiji la Nairobi (NMS), iliyozinduliwa mapema mwaka huu na Rais Uhuru Kenyatta inajikakamua kuimarisha huduma kwa wananchi, hali mbovu ya barabara, misongamano ya mara kwa mara, uchafu katika baadhi ya mitaa, ni miongoni mwa masuala yanayopaswa kuangaziwa kwa kina.

Meja Jenerali Mohamed Badi ndiye Mkurugenzi wa NMS, na kwa kiasi fulani ameonekana kuchapa kazi.

Utendakazi wa Jemedari huyo ukipigiwa upatu na Rais Uhuru Kenyatta na wanaoshuhudia jitihada zake, bidii anazotia zinapaswa kuigwa na atakayerithi Sonko.

Himizo kwa wakazi na wapiga kura wa Nairobi wawe makini watakaposhiriki kuchagua gavana wao wa tatu, wafahamu bayana chaguo lao ndilo litaamua huduma watakazopokea.

Ni kinaya kuona mgombea aliyeondolewa mamlakani kaunti nyingine kwa tuhuma za ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi akiidhinishwa kuwania ugavana Nairobi.

Kipengele cha 180 cha Katiba ya sasa na iliyozinduliwa 2010 kimeweka wazi mahitaji ya mgombea wa kiti cha ugavana na naibu wake.

Hatua ya Ferdinand Waititu kueleza nia yake kumrithi Mike Sonko imezua mdahalo mkali mitandaoni, baadhi wakiikashifu kwa matendo yake wakati akiwa gavana Kiambu na wengine wakimuunga mkono.

Afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa nchini hata hivyo iliidhinisha uhalisia wa Waititu kushiriki kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi.

Nimechoshwa na matukio yanayoshuhudiwa Kenya. Sijui ni matakwa yapi yanazingatiwa na msajili wa vyama vya kisiasa kuidhinisha wawaniaji wa viti vya kisiasa? Umefurushwa afisini kwa sababu ya ufisadi, na chini ya mwaka mmoja unahamia kaunti jirani kuwania wadhifa uliobanduliwa. Kupambana na ufisadi, sharti taasisi husika zionyeshe makali yake. Hatuna imani na wanasiasa wa Kenya.

Waititu kuwania ugavana Nairobi ni utani wa hali ya juu.

 

You can share this post!

Maseneta mbioni kupitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Uhuru atoa amri miradi Kisumu ikamilike upesi